Dortmund yapanda kileleni
2 Novemba 2013Ilikuwa karamu ya magoli kwa Borussia Dortmund makamu bingwa wa ligi ya Ujerumani , Bundesliga , baada ya kuisambaratisha VFB Stuttgart kwa mabao 6-1 katika uwanja wao wa Signal Iduna Park mjini Dortmund jana Ijumaa.
Mshambuliaji Robert Lewandowski alipachika mabao matatu katika kipindi cha pili wakati Borussia Dortmund ikijiweka kileleni mwa msimamo wa ligi, licha ya kuwa ni kwa muda tu, wakati ambapo mabingwa Bayern Munich watakuwa uwanjani hii leo(02.11.2013) kupambana na Hoffenheim, mchezo ambao huenda ukairejesha timu hiyo ya kutoka jimbo la Bavaria kileleni mwa msimamo wa ligi ya Ujerumani.
Mfungaji bora
Mshambuliaji huyo raia wa Poland ambaye hivi sasa anaongoza kwa kufunga mabao tisa katika Bundesliga , alifunga mabao matatu katika muda wa dakika 18 na kuisaidia timu yake kufikisha points 28, mbili mbele ya mabingwa Bayern Munich.
Stuttgart ambayo imepata kipigo chake cha kwanza katika michezo minane ya ligi chini ya kocha wao mpya Thomas Schneider , ilipata bao la kuongoza mapema katika mchezo huo wakati Karim Haggui alipouweka wavuni mpira wa kona uliopigwa na Alexandru Maxim lakini furaha hiyo haikudumu.
Dortmund ambayo itakuwa mwenyeji wa Arsenal London katika Champions League wiki ijayo, ilijibu haraka kwa kufunga mabao mawili ya haraka katika muda wa dakika tatu baada ya kuisambaratisha sehemu ya ulinzi ya Stuttgart kwa kasi yao.
Leo(02.11.2013) Bayer Leverkusen ambayo iko katika nafasi ya tatu, inapambana na Eintracht Braunschweig.
Hamburg SV ina kibarua dhidi ya Borussia Moenchengladbach, na Eintracht Frankfurt ina miadi na Wolfsburg. Katika kinyang'anyiro cha timu zilizo katika nafasi ya chini ya msimamo wa ligi Nüremberg ambayo hadi sasa haijapata ushindi inapambana na Freiburg. Kesho Jumapili ni zamu ya Augsburg ikitiana kifuani na Mainz na Bremen itaoneshana kazi na Hannover.
Ashindwa kutikisa wavu
Katika ligi ya Uhispania , FC Barcelona ilipata ushindi wa jasho pale ilipofanikiwa kuutikisa wazu wa Espanyol mara moja tu katika dakika 90 jana Ijumaa na kuendelea kuwa juu ya msimamo wa ligi hiyo. Messi anapitia kipindi chake kigumu kabisa katika soka baada ya kushindwa kutikisa nyavu katika ligi ya Uhispania tangu mwezi Septemba.
Nchini Ufaransa Paris Saint-Germain ilipata ushindi wa kishindo´ wa mabao 4-0 dhidi ya Lorient jana Ijumaa wakati Edinson Cavani akipachika mabao mawili na kuisaidia timu hiyo kuendelea kubaki kileleni mwa League 1.
Katika Premier League kocha Andre Villas-Boas wa Tottenham Hot Spurs amewaonya wachezaji wake kuwa hatakubali kuteleza tena iwapo timu hiyo inataka kuwamo katika mbio za kuwania ubingwa wa Premier League.
Spurs inakumbana na Everton siku ya Jumapili.
Lakini shughuli inaikabili Arsenal wakati itakapoikaribisha Liverpool leo uwanjani Emirates. Fulham inapambana na Manchester United, Hull City ina miadi na Sunderland, Manchester City inaikaribisha Norwich City , wakati Newcastle ina kibarua na Chelsea.
Pambano lingine la kuvutia kesho Jumapili mbali ya Everton na Spurs ni pambano la kwanza la watani wa jadi kusini mwa Wales katika premier league msimu huu ambapo Swasea inasafiri kwenda Cardiff.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Bruce Amani