Dortmund yatafakari kuruhusu mashabiki uwanjani
4 Juni 2020Mkurugenzi wa klabu ya Borussia Dortmund Michael Zorc amesema wanaangalia kila mbinu ya kuwezesha mashabiki kuingia uwanjani, japo kwa sasa wameridhika na jinsi hali ilivyo.
Hata hivyo haijabainika idadi ya mashabiki ambao wataruhusiwa kuingia katika uwanja wa Signal Iduna Park, wenye uwezo wa kubeba mashabiki 80,000.
Miongoni mwa masuala watakayoyazingatia kabla ya kuwaruhusu mashabiki kuingia uwanjani ni kutokaribiana kwa mashabiki, utaratibu wa kutumia vyoo, namna ya kuingia na kutoka uwanjani, uuzaji wa vyakula miongoni mwa mengine.
Vile vile, Mkurugenzi wa Bayern Munich Oliver Kahn amesema kuwa utaratibu uliowekwa na usimamizi wa soka la Ujerumani unaruhusu mashabiki kati ya 10,000 hadi 11,000 katika uwanja wa Allianz Arena.
Kauli za wadau hao wa soka zinajiri baada ya Hungary kuanza kuwaruhusu mashabiki kuingia uwanjani japo kwa utaratibu maalum. Mashabiki waliruhusiwa kuingia uwanjani kutazama mechi ya fainali iliyochezwa Jumatano (3.05.2020) nchini humo kati ya Honved na Mezokovesd Zsory mjini Budapest.
Hata hivyo, wengi wa mashabiki walionekana kupuuza masharti ya kutokaribiana.
(dpa)