DRC yaahidi kukomboa maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa M23
3 Novemba 2022Kauli hiyo imejiri baada ya waziri wa Ulinzi, Gilbert Kabanda, kusikilizwa Jumatano na Tume za Ulinzi na Usalama za Bunge la Kitaifa na Seneti. Siku hiyo hiyo, Kenya ilitangaza kwamba wanajeshi wake wako tayari kutumwa Kongo.
Waziri wa Ulinzi alikuwa Bungeni ili kutathmini hali jinsi ilivyo katika maeneo ya mkoa wa Kivu Kaskazini ambako mapigano yanaendelea baina ya vikosi vya jeshi la Kongo (FARDC) na waasi wa M23 ambao Umoja wa Mataifa umetambua wanaungwa mkono na Rwanda.
Wakimbizi wa DRC wakimbilia Rwanda
Ni baada ya mkutano huo ndipo Waziri Gilbert Kabanda aliposisitiza kwamba serikali itafanya kila kitu ili kurejesha haraka maeneo ambayo tayari yamedhibitiwa na adui. Hali ambayo bunge linaifuatilia kwa makini, kama alivyoeleza Bertin Mubonzi, mwenyekiti wa Tume ya Ulinzi na Usalama ya Bunge la Kitaifa.
"Sisi kama wawakilishi wa wananchi tunafuatilia kwa karibu sana hali ya wasiwasi huko mashariki na tunasikitishwa na mateso ya raia ambayo yamedumu, na ndiyo maana ilikuwa muhimu kukutana na waziri ili pamoja tutafakari cha kufanya ili jeshi letu kuwa na nguvu ya kutuwezesha, sio tu kushinda vita hivi lakini pia kurejesha amani na usalama," amesema Mubonzi.
Waziri Kabanda aliomba na akapewa masaa 48 ili kujibu hoja za wabunge na maseneta kwani alilazimika kwanza kwenda haraka huko Kivu Kaskazini kwa ufafanuzi zaidi.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inawataja waasi wa M23 ambao kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ni magaidi. Congo imekuwa ikiituhumu Rwanda kuwaungwa mkono waasi hao.
Tshisekedi aiandama Rwanda Umoja wa Mataifa
Jumatano hiyo hiyo, Kenya ilithibitisha kwamba wanajeshi wake ambao wataungana na kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kupambana na waasi mashariki mwa Kongo wako tayari kutumwa. Nilimuuliza Omar Kavota kutoka muungano wa shirika za kiraia mkoani Kivu kaskazini nini wakazi wanachokitarajia kutoka kwa vikosi vya Kenya?
"Tunachotarajia kwa Kenya ni kusaidia majeshi ya Kongo (FARDC) kukomboa maeneo yote ambayo yamekakiwa na vikosi vya wavamizi vya Rwanda ambavyo vinaitwa M23. Tunaomba vikosi hivyo kupigana. Visiwe vinakuja kutazama. Vije pembeni ya FARDC kukomboa maeneo yote ambayo yametekwa na magaidi wa M23 kutoka Rwanda".
Imepita zaidi ya miezi minne tangu M23 kuchukua udhibiti wa Bunagana ambao ni mji muhimu kwenye mpaka na Uganda. Hivi karibuni wamechukua miji mingine ikiwemo Kiwanja na Rumangabo. Lakini jeshi la taifa limedhamiria kurejesha kila kitu.
Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.