1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yaituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23

29 Machi 2022

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeishtumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa kundi la M23 katika mapigano yaliyozuka upya  wilayani Rutshuru na kusabbisha maelfu ya raia kukimbilia nchi jirani ya Uganda.

https://p.dw.com/p/49AHz
M23 Rebellen erobern Goma
Picha: Simone Schlindwein

Akihutubia mkutano wa wanahabari  siku ya Jumatatu kwenye Ikulu ndogo mjini Goma, msemaji wa gavana wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Jenerali Sylvain EKENGE, amedai  kuwa jeshi la Kongo, FARDC limewakamata wanajeshi wawili wa Rwanda waliokuwa wanapigana bega kwa bega na waasi wa M23 dhidi ya jeshi la serikali ya Kongo Jumapili na Jumatatu,  hali inayouweka mashakani uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

M23-Rebellen, Demokratische Republik Kongo
Waasi wa kundi la M23 wakiondoka eneo la Masisi na Sake mwaka 2013Picha: picture-alliance/AP

Hadi wakati huu, waasi wa M23 wameendelea kukita ngome zao kwenye milima ya Chanzu na Runyoni ambako mapigano makali yalishuhudiwa kati yao na jeshi la FARDC, na kusababisha zaidi ya wakaazi Elfu tano kuvuka mpaka wakielekea Uganda na wengine katika vijiji jirani vinavyodhaniwa kuwa na utulivu.

Jeshi la Kongo limehakikisha kwamba hatua zote zimechukuliwa ili kurejesha haraka mamlaka ya serikali na kurejesha amani, kauli ambayo ni tofauti na jinsi hali ilivyo kwa sasa katika vijiji vilivyo baki ukiwa.Uganda yakanusha madai ya Rwanda kuhusu kundi la M23

Kundi hili linalo ishutumu Kinshasa kwa kutoheshimu ahadi zake limekuwa ni tishio kubwa kwa usalama wa wananchi tangu mwaka wa 2013. Asasi za kiraia zimelitaka jeshi la Kongo kuongeza juhudi zake ili kudumisha usalama wa wananchi.

Tokea usiku wa Jumatatu milio ya silaha  nzitonzito imeendelea kusikika katika kijiji cha Chengerero  kando na mji mudogo wa Bunagana wilayani Rutshuru.