1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yawazika waliouawa na wanajeshi kwenye maandamano

19 Septemba 2023

Hatimaye serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewazika watu 57 waliouawa na wanajeshi katika maandamano ya Agosti 30 mjini Goma, huku ikiendelea kuwashikilia waandamanaji wengine zaidi ya 100.

https://p.dw.com/p/4WY8r
DR Kongo Anti-UN-Protesten
Picha: AFP

Baada ya mazungumzo kati yake na baadhi ya ndugu wa watu waliouawa, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kongo Peter Kazadi alithibitisha kuwa waliozikwa jioni ya siku ya Jumatatu (Septemba 18) kwenye makaburi ya Makao yaliyo nje kidogo ya mji wa Goma ni watu 57.

Mwenyewe, Kazidi, alihudhuria mazishi hayo aliyosema yalimtia "huzuni sana."

Wakati maiti zikitolewa kutoka chumba cha kuhifadhia maiti, jamaa wa marehemu hao walisimama kwenye mvua kubwa wakitazama jinsi ndugu zao walivyokuwa wakipangwa kwenye majeneza ya rangi nyeupe.

Soma zaidi: Waliouawa maandamano DRC wazikwa

Mmoja wa ndugu hao, ambaye naye alikuwamo kwenye maandamano ya kupinga kuwepo kwa vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini Kongo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Kahindo, aliiambia DW kwamba walifyatuliwa risasi kwa makusudi na wanajeshi wa nchi yake mwenyewe.

Maandamano ya kupinga 'mazishi ya lazima'

Wakati hayo yakiendelea, ndugu na jamaa wengine walikuwa wakiandamana upande wa magharibi mwa mji wa Goma wakipinga mazishi hayo, wakisema yalifanyika bila ya kushirikishwa na serikali ilichukuwa hatua hiyo bila kwanza kufanya uchunguzi wa mauaji ya ndugu zao.

DR Kongo Proteste im Vorfeld des Gerichtsprozesses gegen Offiziere in Goma
Maandamano yaliyozimwa kwa mauaji dhidi ya raia mjini Goma.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Maandamano ya kupinga kuwepo kwa Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Kongo yalisababisha vifo kadhaa, miongoni mwao wakiwa waumini wa madhehebu ya Kizalendo wanaotaka kikosi hicho kiondoke mara moja nchini humo.

Soma zaidi: DRC: Wakaazi wataka mamlaka kukabidhi maiti kwa familia zao

Katika taarifa nyengine, Rais Felix Tshisekedi amemteuwa Jenerali Peter Chirimwami kuwa gavana mpya wa kijeshi wa jimbo la Kivu Kaskazini, akichukuwa nafasi ya Constant Ndima aliyerejeshwa jijini Kinshasa wiki mbili zilizopita.

Imetayarishwa na Benjamin Kasembe/DW Goma