1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRCongo mabingwa wa kombe la CHAN 2016

Admin.WagnerD8 Februari 2016

DR Congo mabingwa wa kombe la CHAN 2016 , timu kukutana na rais Kabila kesho Jumanne(09.02.2016). Bayern Munich yatoka sare na Leverkusen lakini bado inaongoza ligi

https://p.dw.com/p/1HrdW
Fußball Nationalmannschaft Demokratische Republik Kongo
Timu ya taifa ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo iliyoshiriki mashindano ya kombe la Afrika 2015.Picha: JUNIOR D.KANNAH/AFP/GettyImages

Tukianzia huko barani Afrika, ilikuwa shangwe na vigelele, katika miji ya Goma, Lubumbashi na mji mkuu Kinshasa , pamoja na miji mingine jana Jumapili (07.02.2016)wakati timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo , Chui wa Congo waliponyakua kwa mara ya pili taji la ubingwa wa mataifa ya Afrika linalohusisha wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani maarufu kama CHAN.

Congo iliishinda Mali kwa mabao 3-0 katika uwanja wa mjini Kigali wa Amahoro jana Jumapili.

Nayo Cote D'Ivoire ilikamata nafasi ya tatu katika mashindano hayo baada ya kuibwaga Guinea kwa mabao 2-1, licha ya Guinea kukosa mikwaju miwili ya penalti wakati wa mchezo huo.

Bundesliga

Katika Bundesliga, Bayern Munich iliambulia sare ya bila kufungana siku ya Jumamosi ilipokuwa wageni wa Bayer Leverkusen. Lakini Bayern imeendelea kuongoza ligi hiyo kwa pointi nane zaidi ya timu inayoifuatia. Mlinda mlango wa Bayern Munich Manuel Neuer anasema huo ulikuwa mmoja kati ya michezo waliyotarajia kuwa migumu.

Arsenal gegen Bayern München Fußball Manuel Neuer London Großbritannien
Mlinda mlango wa Bayern Munich Manuel NeuerPicha: Reuters/D.Martinez

"Ndio, bila shaka ulikuwa mchezo tuliotarajia kuwa mgumu. Lakini pamoja na hayo tulionesha uwezo mkubwa. Leverkusen , kama kawaida yao wakiwa nyumbani ama ugenini , wametuweka katika mbinyo mkubwa. Pamoja na hayo lakini , nadhani tulikuwa na fursa nzuri zaidi za ushindi."

Bayern ilionekana kuchanganyikiwa kidogo kutokana na uamuzi wa kocha Pep Guardiola kujiunga na Manchester City msimu ujao wakati timu hiyo ikikabiliwa hivi sasa na majeruhi katika nafasi yake ya ulinzi.

Fußball Bundesliga Schalke 04 vs. VfL Wolfsburg Julian Draxler
Julian Draxler wa VFL WolfsburgPicha: picture-alliance/dpa/G. Kirchner

Schalke 04 ilipanda hadi nafasi ya nne katika msimamo wa ligi , pointi mbili nyuma ya Hertha Berlin , baada ya kuipa kisago VFL Wolfsburg cha mabao 3-0. Mchezaji wa kati wa Wolfsburg Julian Draxler ambaye amehama kutoka Schalke kwenda Wolfsburg msimu huu na ukiwa mchezo wake wa kwanza katika klabu yake ya zamani alikuwa na wakati mgumu na mashabiki wa timu yake ya zamani.

"Bila shaka inauma, lakini nilikuwa nimejitayarisha kwa hilo. Naweza kufahamu hasira za mashabiki. Lakini haikuwa muhimu sana leo , na mwanzoni tu mchezo huo ulikuwa tayari umepata matokeo. Na leo tulicheza vibaya sana , na ndio sababu tumeshindwa kwa mabao 3-0."

Wolfsburg , ambayo msimu uliopita ilikamata nafasi ya pili na ambayo bado imo katika mbio za Champions League , imeporomoka hadi nafasi ya nane baada ya kushindwa kupata ushindi katika michezo yake saba iliyopita.

Fußball Bundesliga 19. Spieltag VfB Stuttgart vs. Hamburger SV
Daniel Didavi wa VFB StuttgartPicha: Getty Images/Bongarts/S. Hofmann

Borussia Dortmund imeendelea kushika nafasi ya pili na kufungua mwanya wa pointi kumi kwa timu inayoifuata ya Hertha BSC Berlin ambayo inashikilia nafasi ya tatu , baada ya timu hizo kutoka sare ya bila kufungana mjini Berlin siku ya Jumamosi.

VFB Stuttgart inaonesha uhai tena baada ya kupata ushindi mara mbili , ambapo siku ya Jumamosi iliirarua Eintracht Frankfurt kwa mabao 4-2 na kuchupa hadi nafasi ya 12.

Fußball EM 2016 Qualifikation Griechenland Färöer
Claudio Ranieri kocha wa Leicester City ya UingerezaPicha: AFP/Getty Images/A. Tzortzinis

Mshambuliaji wa Stuttgart Daniel Didavi anaeleza kwanini timu yake imeendelea kupata matokeo mazuri.

"Nafikiri , wiki chache zilizopita ilikuwa vigumu kufikiri kama itawezekana. Tumeweza hivi sasa , na kwa kiasi fulani tumepata nafasi kutoka chini tulikokuwa. Nafikiri , hakuna mmoja wetu anayeweza kutubeba, lakini ikiwa tutaendelea hivi , basi hali inaonekana kuwa nzuri."

Borussia Moenchengladbach iliirarua Werder Bremen kwa mabao 5-1 na kujisogeza hadi nafasi ya 6.

DFB Pokal robo fainali

Wakati huo huo robo fainali ya kombe la shirikikisho nchini Ujerumani DFB Pokal inafanyika kesho Jumanne na Jumatano, ambapo Borussia Dortmund inaikaribisha VFB Stuttgart , na Bayer Leverkusen inakabana koo na Werder Bremen.

Fußball Chelsea Diego Costa
Diego Costa wa ChelseaPicha: Reuter/Toby Melville

Siku ya Jumatano Bayern Munich inakwenda nyumbani kwa Bochum , wakati Hertha Berlin inakwaana na timu ya daraja la pili ya Heidenheim.

Premier League ya Uingereza

Katika ligi ya Uingereza Premier League , Leicester City imeendeleza uongozi wake juu ya msimamo wa ligi hiyo kwa pointi tano kwa ushindi wa kushangaza wa mabao 3-1 dhidi ya Manchester City , timu ambayo imeporomoka nafasi mbili hadi nafasi ya nne.

Kocha wa Leicester Claudio Ranieri amesema baada ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya Manchester City kwamba mbinyo sasa unaongezeka kwa mahasimu wa timu hiyo kuwaondoa Mbweha hao kutoka kiti cha usukani wa Premier League.

Kombibild Luis van Gaal und Thomas Tuchel
Luis van Gaal (kushoto) wa Manchester UnitedPicha: picture alliance/dpa

Mbinyo ulikuwa kwetu mwanzoni wakati lengo letu lilikuwa kubakia katika ligi , lakini sasa mbinyo uko kwa timu nyingine ambazo zinatumia fedha nyingi kununua wachezaji ili kushinda taji hilo na Champions League, amesema kocha huyo Mtaliani baada ya mchezo.

Manchester United ilijikuta inaachia ushindi nyumbani kwa Chelsea jana wakati Diego Costa alipopachika bao dakika za majeruhi kuipatia timu yake sare ya bao 1-1. Hali hiyo imeiweka Man United pointi sita nyuma ya majirani zao Manchester City.

Lakini mchezaji wa kati wa Manchester United Juan Mata amesema baada ya mchezo huo jana kwamba Manchester imeonesha kwamba inaweza kucheza soka ya kuvutia na kushambulia katika michezo yao ya hivi karibuni. Mchezo wa United umekuwa ukikosolewa sana msimu huu na mchezaji wa kati wa zamani wa timu hiyo Paul Scholes ameueleza kuwa usiovutia na unaochosha kuangalia.

Huku mbinyo ukiongezeka kwa kocha Luis van Gaal , United imeonesha nia thabiti ya kuvunja ulinzi wa timu pinzani katika wiki za hivi karibuni, na kwamba imefungwa tu mara moja katika michezo yao tisa katika mashindano yote.

Barcelona bado haina mshindani

Nchini Uhispania Barcelona ilishinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Levante , ikiwa ni rekodi ya michezo 28 bila kushindwa, na kurejea katika uongozi wake wa pointi tatu mbele ya Atletico Madrid ambayo nayo ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Eibar.

Real Madrid imeendelea kuwa pointi nne nyuma baada ya kibarua kigumu kuiangusha Granada kwa mabao 2-1.

Nchini Italia , Napoli iliendelea kuongoza ligi hiyo Serie A kwa kuishinda Carpi kwa bao 1-0, wakati Juventus Turin iliishinda Frosinone kwa mabao 2-0.

Na nchini Ufaransa Paris St. Germain imeendelea kukata mbuga kuelekea ubingwa wake nchini humo wakati walipoipigisha magoti Olympique de Marseille kwa mabao 2-1.

Kombe la FA

Matayarisho ya Liverpool katika mchezo wa kesho Jumanne wa marudio ya kombe la FA nchini Uingereza dhidi ya West Ham United hayajakuwa mazuri kutokana na kocha wao Juergen Klopp kufanyiwa upasuaji , pamoja na majeruhi lukuki katika kikosi hicho, na pia uasi wa mashabiki dhidi ya viongozi wa klabu hiyo kwa kupandisha bei ya tikiti. Hali ya kocha huyo wa Liverpool inaendelea vizuri na anapanga kurejea tena katika benchi la ufundi la kikosi hicho leo Jumatatu saa 48 baada ya opereshni kuondoa kidole cha tumbo , imesema ripoti kutoka klabu hiyo.

Siku ya Jumatano kutakuwa na mpambano wa nusu fainali ya kombe la Uhispania , lakini Barcelona haionekani tena kuwa katika hatari baada ya kuirarua Valencia wiki iliyopita kwa mabao 7-0. Seville pia itaingia katika mchezo mwingine wa nusu fainali siku ya Alhamis kifua mbele ikiwa mbele kwa mabao 4-0 dhidi ya Celta Vigo.

Riadha na kashfa ya Doping

Kwa upande wa Riadha , kiongozi wa shirikisho la vyama vya riadha duniani IAAF Sebastian Coe amekiri leo kwamba hakuna nafasi ya kurekebisha mambo kwa haraka wakati akijaribu kurejesha imani ya mashabiki wa mchezo huo uliokumbwa na matatizi makubwa .

Lakini Coe mwenye umri wa miaka 59 , akiwa katika ziara nchini Japan kama mwenyekiti wa chama cha Olimpiki cha Uingereza BOA, ameahidi kutoa jukwaa lililo safi kwa wanariadha walio safi.

England Sebastian Coe
Sebastian Coe rais wa IAAFPicha: imago/ZUMA Press

Amesema kwamba , namnukuu," kama nilivyosema kabla, safari ya kurejesha imani haina hakika ya urefu wake, lakini tunapaswa kufanya mabadiliko."

Wakati huo huo kamati ya olimpiki ya Marekani imevieleza vyama vya michezo nchini humo kwamba wanariadha na viongozi wenye wasi wasi wa afya zao kuhusiana na virusi vya Zika wanapaswa kufikiria kutokwenda katika michezo ya Olimpiki mwaka huu itakayofanyika mjini Rio de Janeiro nchini Brazil mwezi Agosti.

Ujumbe huo ulitolewa katika mkutano uliohusisha maafisa wa kamati ya Olimpiki nchini Marekani na viongozi wa michezo nchini humo mwishoni mwa Januari, kwa mujibu wa watu walioshiriki katika mkutano huo.

Mwandishi : Sekione kitojo / rtre / dpae / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman