1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Dunia yalaani mapinduzi ya kijeshi Myanmar

1 Februari 2021

Umoja wa Mataifa, Marekani na mataifa kadhaa ulimwenguni yamelaani mapinduzi ya kijeshi nchini Myanmar yakitowa wito wa kurejeshwa utawala wa kidemokrasia na kuachiliwa huru Aung San Suu Kyi na wanasiasa wenzake.

https://p.dw.com/p/3of91
Myanmar  General Min Aung Hlaing
Picha: Soe Zeya Tun/REUTERS

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres, amelaani vikali kushikiliwa kwenye mahabusu za kijeshi kwa Aung San Suu Kyi, Rais Win Myint na viongozi wengine wa kiraia, kufuatia mapinduzi hayo ya kijeshi mapema Jumatatu (Februari 1).

Msemaji wa katibu mkuu huyo, Stephane Dujarric, amesema kwamba matukio haya "yanaashiria pigo kubwa kwa mageuzi ya kidemokrasia" nchini Myanmar. 

Msemaji wa Ikulu ya White House, Jan Psaki, alisema kwenye taarifa yake kwamba Marekani itachukuwa hatua kali dhidi ya wale waliohusika na mapinduzi hayo, endapo hawakuuresha haraka utawala wa kiraia.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, Marekani "haikubaliani na jaribio lolote la kuyapinduwa matokeo ya uchaguzi wa mwezi Novemba", ambao ulikipa chama cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi ushindi mkubwa kabisa, lakini ukakumbwa na tuhuma za wizi wa kura.

Waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken, naye pia alitoa tamko rasmi kulitaka jeshi la Myanmar kuwaachia huru maafisa wote wa serikali na asasi za kiraia waliowakamata, pamoja na kuheshimu matakwa ya watu wa Myanmar kupitia uchaguzi wa Novemba 8.

Jeshi latakiwa kuheshimu maamuzi ya raia

Myanmar Militärputsch
Mwanajeshi akiwa amesimama kwenye kizuizi cha barabarani kuelekea bunge la Mnyanmar mjini Naypyidaw siku ya tarehe 1 Februari 2021, kufuatia mapinduzi ya kijeshi.Picha: AFP via Getty Images

Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, naye alilaani mapinduzi hayo ya kijeshi na pia kutowa wito wa kuachiliwa kwa watu wote wanaoshikiliwa. "Serikali halali ya kiraia inapaswa kurejeshwa kwa kuzingatia katiba ya nchi na uchaguzi wa Novemba," aliandika rais huyo wa kamisheni ya Ulaya kwenye mtandao wa Twitter.

Kabla ya mapinduzi hayo, mnamo tarehe 29 Januari, Marekani pamoja na mataifa mengine ya Magharibi yalitowa tamko la pamoja kulitaka jeshi kuheshimu utamaduni wa kidemokrasia, kufuatia kitisho kilichotolewa na amiri mkuu wa majeshi ya Myanmar kwamba angelisitisha kutumika kwa katiba ya nchi.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alilaani mapinduzi hayo na kushikiliwa kwa Aung San Suu Kyi. Kupitia ujumbe wake wa Twitter: "Kura ya wananchi lazima iheshimiwe na viongozi wa kiraia waachiliwe."

China, ambayo kawaida hupinga uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar, imetaka pande zote kutatuwa mkwamo uliopo.

"China ni jirani rafiki wa Mnyanmar na tunarajia pande mbalimbali zinazohusika na mgogoro huu kuutatuwa kwa kufuata katiba na sheria za nchi yao ili kulinda utulivu wa kisiasa na kijamii." Msemaji wake wa mambo wa kigeni, Wang Wenbin, alisema kwenye taarifa yake, ambapo kauli kama hiyo imetolewa pia na Japan, Uturuki, Canada, Singapore na Norway.

Hadi kufikia mchana wa Jumatatu, hakukuwa na taarifa za majaaliwa ya Aung San Suu Kyi na wenzake walioshikiliwa.