1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yampongeza Johnson kwa tahadhari

13 Desemba 2019

Wakati viongozi duniani wanaendelea kumpongeza Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kwa ushindi mkubwa wa chama chake, Umoja wa Ulaya unasema unataka mazungumzo ya haraka kulimaliza suala la kujitoa kwenye umoja huo

https://p.dw.com/p/3UlhJ
Großbritannien Boris Johnson nach der Wahl 2019
Picha: Reuters/D. Martinez

Rais Donald Trump wa Marekani amesema baada ya ushindi huu wa Johnson, sasa Marekani na Uingereza zitaweza haraka kufanikisha makubaliano ya kibiashara baada ya Uingereza kujiiondoa kwenye Umoj wa Ulaya.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa licha ya kumpongeza Johnson, lakini ameonya kuwa hatua yoyote ya Uingereza kujiondoa kwenye kanuni za kibiashara na Umoja wa Ulaya zitamaanisha kuwa nchi hiyo italipoteza soko zima la Ulaya.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameuita ushindi wa Johnson kuwa wa wazi, huku akiahidi kufanya kazi naye kutokana na urafiki na ushirikiano wa muda mrefu baina ya mataifa yao mawili, kwa mujibu wa ujumbe wa Twitter uliotumwa na msemaji wa Merkel, Steffen Seibert.

Salamu kama hizo zilitumwa na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, ambaye naye alisema anatarajia mashirikiano ya karibu kuendelezwa na serikali zao mbili. India iliwahi kuwa koloni la muda mrefu la Uingereza.

Huko mjini Brussels, kwenye makao makuu ya Muungano wa Ulaya, Waziri Mkuu wa Ireland, Leo Varadkar, naye alimpongeza Johnson, akisema ushindi huo ni muhimu kwa kwake mwenyewe Johnson na pia kwa chama chake. "Ninadhani ni jambo zuri kwamba sasa tuna matokeo yanayoonesha uamuzi wa wazi wa Uingereza." Alisema.

EU yataka suala la Brexit limalizike haraka

Belgien Premierminister Charles Michel
Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel.Picha: AFP/G. van der Hasselt

Ama kwa Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, ushindi huu wa Johnson una maana moja tu muhimu: nayo ni njia ya kuumaliza mkwamo wa siku nyingi kwenye suala la Uingereza kujiondoa kwenye Muungano wa Ulaya, maarufu kama Brexit, ambalo ndilo hasa lililopigiwa kura na Waingereza kwenye uchaguzi huo wa jana.

"Napenda kumpongeza Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, kwa ushindi wake. Na sasa tunatarajia Bunge la Uingereza litayapigia kura haraka iwezekanavyo makubaliano ya kujitoa kwenye Muungano wa Ulaya. Ni muhimu kuwa na uwazi haraka iwezekanavyo na sisi tuko tayari," alisema Michel.

Katika miji mingi mikuu hapa Ulaya hivi leo, vyombo vya habari vimeukaribisha ule viliosema ni mwisho wa mkwamo, lakini kwa mashaka makubwa. Gazeti la Frankfurter Allgemeine limehoji endapo ushindi wa Johnson umekuja kwa gharama gani, kwani linahofia kuwa matokeo haya huenda yasiwapatie chochote tafauti ya kile kilichopigiwa debe na propaganda za kuondoka muungano wa Ulaya.

"Vita hasa na Brussels ndio kwanza vimeanza", limeandika gazeti la Ilta-Sanomat la Finland, huku lile la De Volkskrant la Uholanzi likisema ingawa ushindi huo ni ahuweni kwa Johnson lakini ni changamoto kwa muungano ndani ya Uingereza yenyewe.