Dunia yasubiri kwa hamu mkutano wa Trump na Kim
11 Juni 2018Kauli ya Trump imekuja mnamo ambapo maafisa wa pande zote walipokutana ili kupunguza tofauti zao juu ya namna gani ya kumaliza mkwamo juu ya nyuklia kwenye Rasi ya Korea. Hata hivyo mkutano huo umegubikwa na masuala yaliyojitokeza katika mkutano wa kilele wa nchi saba zilizoendelea kiviwanda uliofanyika nchini Canada.
Kim na Trump waliwasili Singapore siku ya Jumapili katika nyakati tafauti wakitarajiwa kukutana ana kwa ana, kwa mara ya kwanza. Utakuwa mkutano wa kihistoria baina ya viongozi wa mataifa hayo mawili ambayo yamekuwa na uadui tangu vita ya Korea ya mwaka 1950-1953. Pamoja na ugumu uliosalia juu ya nini kitatokea kuhusu kumalizwa kwa shughuli za nyukilia, maafisa kutoka pande zote walifanya mazungumzo ya masaa mawili ili kusukuma mbele ajenda kuelekea mkutano huo wa kesho.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alisema katika taarifa yake kwamba mikutano hiyo ilikuwa ya "misingi na ya kina" lakini hapakuwa na maelezo kuhusu matokeo yake. Trump alionekana kuwa mwenye mtazamo chanya katika mkutano wake na waziri mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong.
Lakini wakati ambapo ulimwengu ukisubiria kwa shauku mkutano wa kesho baina ya Trump na Kim, rais huyo wa Marekani ameendeleza mashambulizi kupitia ukurasa wake wa Twitter, na kuwatia hasira washirika wake wa Jumuiya ya Kujihami ya nchi za Magharibi NATO, Umoja wa Ulaya na waziri mkuu wa Canada Justin Trueau, katikati mwa mkutano uliogawika wa viongozi wa kundi la nchi saba zilizoendelea kiuchumi G7 uliofanyika mwishoni mwa juma.
Kuongezeka kwa mvutano juu ya biashara baina ya Washington na baadhi ya washirika wake wa karibu duniani, kunatia ukungu juu ya jitihada za Trump za kufanya mkutano wa kihistoria kuhusu mazungumzo ya nyuklia nchini Singapore na kiongozi wa Korea Kaskazini.
Akiwa ameondoka kwenye mkutano wa G7 nchini Canada mapema, Trump alitanga kutounga mkono taarifa ya pamoja ya viongozi hao na kuharibu kile kilichonekana kuwa makubaliano dhaifu juu ya mgogoro wa biashara baina ya Washington na washirika wake wakuu.
Trump alisema kwamba, "biashara ya haki sasa itaitwa biashara ya kijinga ikiwa hakuna makubaliano", akiongeza kwamba hawawezi kuruhusu marafiki zao au maadui wafaidike na biashara za Marekani tena. "Ni lazima tuiweke Marekani kwanza".
Taarifa ya pamoja iliyoonekana kufukia mpasuko uliojitokeza katika mkutano wa G7, ilisema kwamba viongozi wa Marekani, Canada, Uingereza, Ufaransa, Italia, Ujerumani na Japan, walikubaliana juu ya uwepo wa biashara huru, haki na iliyo na maslahi kwa pande zote na umuhimu wa kulinda viwanda vya ndani.
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Peter Altmaier, amesema leo kwamba matukio katika mkutano wa kilele wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda, yamewaleta karibu zaidi viongozi wa Umoja wa Ulaya.
Waziri Altmaier alisema wakati akiwasili Luxembourg kwenye mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya, kwamba mvutano katika mkutano wa kilele wa G7 nchini Canada uliuweka Umoja wa Ulaya karibu zaidi na kusisitiza ni muhimu kuwa na mshikamano katika ngazi zote.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/reuters/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman