Dunia yataka Korea Kaskazini iadhibiwe
8 Februari 2016Tamko la kikao cha dharura cha Baraza la Usalama hapo jana limesema hatua ya Korea Kaskazini kurusha kombora hilo la masafa marefu linakiuka vikwazo vilivyowekwa na Baraza hilo, na pia ni "uchokozi usiovumilika".
Kiongozi wa Korea Kaskazini aliendelea na mipango ya kurusha kombora hilo licha ya maombi ya rafiki yake pekee kwenye eneo hilo, China, ambayo ilikuwa imemtaka kuachana na mpango huo.
Taarifa iliyotolewa baadaye na serikali ya Kim Jong Un ilisema kuwa nchi hiyo ilikuwa imefanikiwa kutuma kifaa cha uchunguzi kwenye satalaiti yake angani, likiwa ni jaribio la pili linalokosolewa na jumuiya ya kimataifa ndani ya mwezi mmoja.
Mwezi uliopita, Korea Kaskazini ilifanya majaribio ya bomu lake la nyuklia, ingawa baadhi ya wachambuzi wa silaha kali wanadai jaribio hilo halikuwa la kweli.
Hivi leo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Fumio Kishida, amesema tamko la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni muhimu lakini lazima liendane na vitendo.
"Baraza la Usalama limetumia kauli kali zaidi kuliko lilivyofanya mwezi uliopita baada ya jaribio la bomu la nyuklia. Sasa ni muda wa kuharakisha mijadala yake na kupitisha azimio lenye uzito mara moja. Japan itaendelea kushirikiana na mataifa yanayotaka kufikiwa lengo hilo kama inavyohitajika," Kishida aliwaambia waandishi wa habari nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.
Australia kuchukuwa hatua kali
Kikao hicho cha dharura cha Baraza la Usalama kilikuwa kimeitishwa na Japan, Marekani na Korea Kusini, na baadaye imefahamika kuwa huenda Marekani ikaharakisha kuweka mtambo wake wa silaha katika Rasi ya Korea baada ya jaribio hilo la Korea Kaskazini.
Nchini Australia, taifa lililo umbali wa kilomita 7,000 kutoka Korea Kaskazini, imesema uamuzi wa Baraza la Usalama dhidi ya Korea Kaskazini unapaswa kutekelezwa kikamilifu, kwani nchi hiyo imekuwa kitisho dhidi ya ulimwengu. Akizungumza bungeni hivi leo, Waziri wa Mambo ya Nje, Julia Bishop, alisema serikali yake itaweka vikwazo zaidi ya vile ambavyo vimeamuliwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini.
"Serikali ya Australia itaendelea kupigania hatua kali zaidi dhidi ya Korea Kaskazini, madhali tu imeendelea na vitendo vyake ambavyo sio tu vinatishia amani na usalama wa eneo hili, bali pia amani na usalama wa dunia. Utawala huu lazima ukomeshwe kwa tabia hii," alisema Bishop kwenye bunge la nchi hiyo.
Australia ambayo ina uhusiano wa kibalozi na Korea Kaskazini, tayari imepiga marufuku biashara ya vitu vya anasa, vifaa na huduma za kijeshi na nchi hiyo, na pia imewapiga baadhi ya Wakorea na mashirika yao kuingia Australia au kushirikiana nao kwa masuala yoyote ya kifedha.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Josephat Charo