1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yayakataa maelezo ya Saudi Arabia kuhusu Khashoggi

21 Oktoba 2018

Ujerumani, Marekani na Canada zaungana na Uturuki na Uingereza kuyashuku maelezo yaliyotolewa na ufalme wa Saudi Arabia juu ya kifo cha mwandishi habari Jamal Khashoggi kwenye ubalozi mdogo wa Saudia mjini Instabul.

https://p.dw.com/p/36tfz
Türkei Istanbul Konsulat Saudi-Arabien | Untersuchungen Jamal Khashoggi
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/A. Bolat

Kwenye taarifa ya pamoja kati yake na Waziri wa Mambo ya Ndani Heiko Maas, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema analaani mauaji hayo na kwamba maelezo yaliyotolewa juu ya kile kilichotokezea kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjinji Istanbul hayatoshi.

Waziri Maas alisema baada ya mazungumzo yake na Kansela Merkel siku ya Jumamosi (21 Oktoba) kwamba hakutakuwa na sababu ya kuendelea na mpango wa kuiuzia silaha Saudi Arabia kabla ya uchunguzi kamili wa kilichomsibu Khashoggi haujawekwa hadharani na waliohusika kuchukuliwa hatua.

Kwa upande wake, wizara ya nje ya Canada imesema kuwa maelezo yaliyotolewa na Saudi Arabia yanakinzana na uhalisia na hayawezi kuaminika, na imetoa wito wa uchunguzi wa kina. 

"Canada inalaani mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashogi, ambayo Ufalme wa Saudi Arabia umeyathibitisha kutokea kwenye ubalozi wake mdogo mjini Istanbul. Maelezo yaliyotolewa hayana uwiano wala uhalali." Ilisema taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Chrystia Freeland.

Trump abadili tena kauli

Türkei Fahne Saudi Arabins über dem Konsulat in Istanbul
Bendera ya Saudi Arabia ikipepea kwenye ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki.Picha: Reuters/M. Sezer

Kauli ya Freeland ilitafautiana na ile iliyotolewa awali ya Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye alikuwa amesema maelezo ya Saudi Arabia yalikuwa ya kweli, kabla ya baadaye naye kubadili kauli yake akisema hakuridhishwa nayo na kwamba alitaka ufafanuzi zaidi. 

Wizara ya Nje ya Uingereza ilielezea kushitushwa kwake na ithibati iliyotolewa na Saudi Arabia kwamba Khashoggi aliuawa kwenye ubalozi wake mdogo nchini Uturuki, baada ya mahojiano yake na maofisa kugeuka mapigano, ikisema kuwa inafikiria hatua za kuchukuwa. 

Tayari vyama vya upinzani vya Labour na Liberal Democrats vimetaka Uingereza isitishe mauzo ya silaha kwa ufalme wa Saudi Arabia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alielezea kukerwa kwake sana na kifo hicho, huku msemaji wake, Stephane Dujarric, akisema kuwa Guterres anataka uchunguzi wa kina na wa wazi na kuwajibishwa waliohusika na mauaji hayo.

Mashirika ya kimataifa yataka uchunguzi huru

Jamal Khashoggi
Marehemu Jamal Khashoggi wakati wa uhai wake.Picha: picture-alliance/AP Photo/V. Mayo

Shirika la haki za binaadamu la Amnesty International lilisema kuwa Saudi Arabia inapaswa kuutoa mara moja mwili wa Khashoggi ili "wataalamu huru wa uchunguzi wafanye upasuaji unaokwendana na viwango vya kimataifa." 

Mkuu wa jumuiya ya vyombo vya habari ya Uturuki, Turan Kislakci, alitoa wito wa mamlaka iliyotoa amri ya kuuawa kwa Khashoggi lazima iadhibiwe. Akizungumza nje ya ubalozi mdogo wa Saudia siku ya Jumamosi, Kislakci alisema mkosoaji huyo wa utawala wa mwanamfalme wa Saudia, Mohammed Bin Salman, aliuawa na wauaji washenzi na kwamba jumuiya yao inataka kuona haki ikitendeka.

Tayari naibu mkuu wa chama tawala cha Uturuki, Numan Kurtulmus, amesema kuwa nchi yake haikubaliani na kulifunikafunika suala hili na kwamba hivi karibuni itaweka hadharani matokeo ya uchunguzi wake, akisisitiza kuwa haiwezekani kwa Saudi Arabia kujichunguza yenyewe kwenye suala ambalo inashukiwa nalo.

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki alitazamiwa kuzungumza kwenye ufunguzi wa uwanja wa michezo jioni ya Jumamosi, ingawa haikufahamika endapo angelizungumzia mauaji hayo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/dpa
Mhariri: Yusra Buwayhid