1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duru ya pili ya Brexit yaanza

17 Julai 2017

Wasuluhishi kutoka Baraza la Umoja wa Ulaya na Uingereza wamekutana Brussels wakati duru ya pili ya mazungumzo inapoanza ya majadiliano rasmi kuhusu masharti ya kujiondoa kwa Uingereza kutoka EU ifikapo mwezi Machi, 2019

https://p.dw.com/p/2ggxK
Brüssel Brexit-Verhandlungen, David Davis & Michel Barnier
Picha: Reuters/Y. Herman

Uingereza, ambayo ni mwanachama wa Umoja huo tangu mwaka 1973, ni taifa la kwanza katika historia ya EU kujiondoa, baada ya kura ya maoni iliyofanyika mwaka jana. 

Pande zote zinahitaji kukubaliana kuhusiana na haki za uraia, suala la mpaka kati ya Uingereza na Ireland Kaskazini, pamoja na majukumu ya kifedha yatokanayo na uanachama wa Uingereza, kabla hawajendelea na mazungumzo ya mustakabali wa mahusiano ya kibiashara.

Baada ya mkutano wa awali mwezi uliopita ambapo kuliandaliwa muundo wa mazungumzo, waziri wa Uingereza kuhusu mchakato huo wa Brexit David Davis alikutana na mjumbe wa majadiliano wa Umoja wa Ulaya kuhusu Brexit Michel Barnier leo kwa ajili ya mashauriano yatakayodumu kwa siku nne zijazo.

"Tunahitaji kuchunguza na kulinganisha nafasi zetu ili kupiga hatua nzuri, amesema  Barnier kabla ya kuanza kwa mkutano, huku Davis akisema wanakaribia kufikia suala la msingi.

Hatua zilizopigwa kuhusu haki za raia wa Umoja wa Ulaya ni mojawapo ya masuala matatu makuu ambayo sharti yasuluhishwe kabla ya pande hizo mbili kuanza kujadili suala pana la mikataba ya kibiashara. 

Belgien Brüssel Start der Brexitverhandlungen
Mazungumzo ya Brexit yanayoendelea mjini Brussels.Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Dunand

Pendekezo la Uingereza linawapa raia wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ambao wameishi Uingerezea kwa takriban miaka miaka mitano haki ya kuishi huko, kufanya kazi na kupata mafao. Kiasi ya raia milioni tatu wa Umoja wa Ulaya walioko nchini humo watahitajika kuwasilisha maombi ya kupewa kibali cha kuishi Uingereza na bado haijabanikia wazi hatma ya wale ambao wameishi kwa muda mfupi nchini humo au ni haki zipi jamaa zao watakuwa nazo Uingereza.

Serikali ya Uingereza bado yajikanganya kuhusu Brexit.

Maafisa wa Umoja wa Ulaya wamesema mapendekezo ya Uingereza hayakidhii mahitaji yote wanayotaka. Bunge la Umoja wa Ulaya wiki iliyopita lilionya kuwa huenda likapiga kura kupinga makubaliano ya mwisho kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza ya mazungumzo ya Brexit iwapo Uingereza haitawapa raia wa Umoja huo haki zaidi iwapo wataamua kuishi nchini humo baada ya nchi hiyo kujiondoa rasmi kutoka Umoja wa Ulaya.

Suala hilo ndilo la kwanza kujadiliwa katika kipindi cha siku nne zijazo za mazungumzo ya Brexit yaliyoanza leo. Kile kitakachoibuka katika mazungumzo hayo pia kitaamua hatma ya Waingereza takriban milioni moja wanaoishi katika nchi za Umoja wa Ulaya.

Davis amesema ni muhimu kwa mazungumzo hayo kupiga hatua za tija wakati huu. Baada ya ufunguzi wa mazungumzo hayo mjini Brussels, waziri huyo wa Uingereza kuhusu Brexit amerejea London na anatarajiwa kurejea Brussels Alhamisi kufanya mkutano na wanahabari wakiwa na Barnier.

Katika mkutano tofauti mjini Bruessels wa mawaziri wa mambo ya nje, Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson amesisitiza kuwa mapendekezo yaliyotolewa na waziri mkuu Theresa May kwa raia wa nchi za Umoja wa Ulaya ni mazuri na yaliyozingatia haki.

Mwaka mmoja baada ya Uingereza kupiga kura ya maoni kujiondoa Umoja wa Ulaya, serikali ya Uingereza inaonekana kujikanganya kuhusu masharti ya kujiondoa. Mawaziri wa utawala wa Theresa May wanatofautiana vikali kuhusu suala hilo la Brexit na kuwatia wasiwasi maafisa wa Umoja wa Ulaya wanaosisitiza miezi ishirini ni muda mfupi wa kufikia makubaliano ya kujiondoa rasmi kwa Uingereza katika njia iliyo na mpangilio.

Mwandishi: Lilian Mtono/ap/Reuters
Mhariri; Saumu Yusuf