1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duru ya pili ya Uchaguzi yafanyika nchini Liberia

8 Novemba 2011

Huku Raia wa Liberia wakiendelea kupiga kura katika duru ya pili ya urais, hali ya wasiwasi imetanda nchini humo kwa kuhofia ghasia za baada ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/136m4
Rais wa Liberia Ellen Johnson SirleafPicha: DW

Idadi ya watu ni ndogo katika vituo vingi vya kupigia kura nchini humo, kinyume na idadi kubwa ya watu waliojitokeza katika upigaji kura wa duru ya kwanza uliofanyika mapema mwezi uliopita.

Baadhi ya wapiga kura wamesema hawatapiga kura katika duru hii ya pili ya uchaguzi wakati huu ambapo kunaonekana kuwa na tishio kubwa la kutokea kwa ghasia.

Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobeli anatarajiwa kushinda uchaguzi huu kufuatia kuongoza kwake katika duru ya kwanza kwa asilimia 44 ya kura.

Katika duru hiyo ya kwanza, mgombea wa urais wa upinzani Winston Tubman, alijipatia silimia 33 ya kura.Raia wa Liberia milioni 1.8 walipiga kura katika duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi.

Uchaguzi huu ni wa pili kufanyika tangu kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka kumi na minne nchini Liberia na kusababisha vifo vya watu nusu millioni, na kuharibu miundo mbinu na kuuvuruga uchumi wa nchi hiyo.

Liberia Wahlen in Monrovia Winston Tubman
Mgombea wa urais kwa tiketi ya CDC Winston TubmanPicha: DW

Huku hayo yakiarifiwa mtu mmoja aliuawa mjini Monrovia hapo jana baada ya mapigano makali kati ya wafuasi wa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha CDC Winston Tubman na vikosi vya serikali pamoja na vile vya Umoja wa Mataifa. Afisa mmoja wa polisi nchini humo alikamatwa na vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa baada ya kukiri kufyatua risasi katika mapigano hayo. Hata hivyo usalama umeimarishwa mjini humo.

Tayari shirika la kutetea haki za kibinaadam la Human Rights Watch limeitisha uchunguzi wa kifo hicho huku wakitoa ujumbe kuwataka raia kudumisha amani katika kipindi hiki kigumu cha uchaguzi.

Naye rais wa Marekani Barrack Obama ametaka vikosi vya usalama Liberia kujaribu kusitisha ghasia na kuweka amani wakati wa shughuli nzima ya uchaguzi. Obama amesema jumuiya ya kimataifa itatoa adhabu kali kwa wale wanaojaribu kuvuruga amani wakati huu wa uchaguzi.

Mgombea wa urais wa upinzani Winston Tubman, katika duru ya kwanza ya uchaguzi alijipatia silimia 33 ya kura.

Mwandishi: Amina Abubakar RTRE/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdulrahman