1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo yanaendelea ili kusitisha mapigano Gaza

9 Novemba 2023

Duru kadhaa zimearifu leo kuwa mazungumzo yanaendelea ili kusitisha mapigano kwa muda wa siku tatu kwenye Ukanda wa Gaza kwa ahadi kwamba wanamgambo wa Hamas watawaachia huru mateka kadhaa inawaowashikilia.

https://p.dw.com/p/4Ybff
Moshi ukienea kaskazini mwa Ukanda wa Gaza
Moshi ukienea kaskazini mwa Ukanda wa GazaPicha: Ammar Awad/REUTERS

Hayo yameelezwa na maafisa wawili wa Misri, mwingine kutoka Umoja wa Mataifa na mwanadiplomasia mmoja wa mataifa ya magharibi walipozungumza na shirika la habari la Associated Press kwa sharti la kutotajwa majina.

Vyanzo hivyo vimesema mazungumzo hayo yanasimimawa kwa pamoja na mataifa matatu ya Qatar, Misri na Marekani.

Makubaliano yanayotizamiwa yatawezesha msaada zaidi kupelekwa Ukanda wa Gaza ikiwemo kiwango kidogo cha mafuta ya petroli ili kupunguza madhila yanayowakumba Wapalestina milioni 2.3 wanaoshuhudia hujuma nzito za kijeshi kutoka Israel inayopambana kulitokomeza kundi la Hamas.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema usitishaji wowote wa vita ni sharti uambatane na kuachiwa huru kwa watu waliochukuliwa mateka na Hamas wakati wa shambulizi la kundi hilo ndani ya ardhi ya Israel mnamo Oktoba 7.