ECOWAS yaakhirisha mkutano wa kijeshi juu ya Niger
12 Agosti 2023Wakuu wa majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) walikuwa wakutane siku ya Jumamosi (Agosti 12) katika mji mkuu wa Ghana, Accra, lakini jioni ya Ijumaa kulitolewa tamko la kuuakhirisha mkutano huo kwa muda usiojulikana, kwa mujibu wa vyanzo vya kijeshi kwenye jumuiya hiyo.
Vyanzo hivyo vilisema mkutano huo ulikuwa umeandaliwa ili kuwaeleza viongozi wa ECOWAS juu ya "njia bora zaidi" za kuunda na kutuma kikosi hicho cha dharura nchini Niger.
Bado ECOWAS haijafafanuwa undani wa kikosi hicho wala ratiba ya hatua zake, huku viongozi wake wakisisitiza kuwa bado wanataka suluhisho la amani.
Soma zaidi: Niger yavunja makubaliano ya kijeshi na Ufaransa
Akhirisho la mkutano huo lilitangazwa wakati maelfu ya wananchi wa Niger wakikusanyika kuunga mkono jeshi lao mbele ya kituo kimoja cha jeshi la Ufaransa jana Ijumaa.
Mkoloni huyo wa zamani ana wanajeshi zaidi ya 1,500 wanaoshiriki kile kinachoitwa "vita dhidi ya makundi ya kigaidi" kwenye taifa hilo la Ukanda wa Sahel.
Wasiwasi wa kutumika nguvu dhidi ya utawala wa kijeshi wa Niger
Tangu mwaka 1990, ECOWAS yenye wanachama 15 imewahi kuingilia kijeshi kwenye mataifa sita miongoni mwa wanachama wake nyakati za vita vya wenyewe kwa wenyewe, uasi ama mkwamo wa kisiasa.
Lakini uwezekano wa kuingilia kijeshi kwenye taifa ambalo tangu awali lipo kwenye hali tete kama Niger umezusha mjadala mkubwa miongoni mwa viongozi wa jumuiya hiyo na onyo la tahadhari kutoka kwa majirani kama vile Algeria na mataifa ya nje kama vile Urusi.
Moscow, ambayo ushawishi wake kwenye ukanda huo umekuwa ukiongezeka, ilisema matumizi ya nguvu za kijeshi yanaweza "kuutanuwa mzozo wenyewe ndani ya Niger na kulisambaratisha eneo zima la Sahel."
Soma zaidi: Maelfu ya watu waandamana Niger kupinga vikwazo vya ECOWAS
Rais Jose Maria Neves wa Cape Verde alisema siku ya Ijumaa kwamba anapingana na uingiliaji kati kijeshi na kwamba nchi yake haitashiriki kwenye kampeni kama hiyo.
Tayari Mali na Burkina Faso, ambazo zenyewe ziko mikononi mwa tawala za kijeshi, zilishaonya kwamba uvamizi wowote dhidi ya Niger ungelichukuliwa kuwa "tangazo la vita" kwa wao pia.
Waziri mpya wa ulinzi wa Niger, Jenerali Salifou Mody, aliitembelea Mali siku ya Ijumaa kwa muda mfupi, kwa mujibu wa mshauri wa rais wa Mali.
Mapinduzi ya Niger ni ya tano tangu taifa hilo kupata uhuru wake kutoka Ufaransa mwaka 1960.
Kama zilivyo Mali na Burkina Faso, nchi hiyo nayo inapambana na uasi wa makundi ya siasa kali ambayo yameshaangamiza maisha ya maelfu ya watu na kuwasababisha mamilioni ya wengine kukimbia makaazi yao, jambo ambalo limeondosha imani ya wananchi kwa serikali zao.
Hali ya Bazoum yazusha mashaka kwenye jumuiya ya kimataifa
Umoja wa Afrika umeungana na Umoja wa Ulaya na Marekani kuelezea wasiwasi wao juu ya hali ya rais wa Niger aliyepinduliwa, Mohamed Bazoum. Kwenye tamko lake, Umoja wa Afrika ulisema siku ya Ijumaa kwamba kutendewa vibaya kwa kiongozi huyo aliyechaguliwa kidemokrasia hakukubaliki.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, alisema walikuwa na taarifa kuwa Bazoum na familia yake wamekuwa wakinyimwa chakula, umeme, na huduma za afya kwa siku kadhaa sasa.
Mkuu wa haki wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, alisema hali anayozuiliwa Bazoum "ni sawa na udhalilishaji wa ubinaadamu unaokwenda kinyume na sheria za kimataifa za haki za binaadamu."
Soma zaidi: Hali ya Bazoum yaitia wasiwasi Jumuiya ya Kimataifa
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Annalena Baerbock, alisema "wapangaji wa mapinduzi wanaweza kukabiliwa na hatua kali endapo jambo lolote baya litamtokea Bazoum na familia yake."
Kauli kama hiyo ilitolewa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, ambaye alisema viongozi wa kijeshi wa Niger wamekataa kuiachilia familia ya Bazoum kama ishara ya nia njema.
Bazoum, mkewe na mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka 20, anayesemekana kuwa na matatizo ya moyo, wako mikononi mwa jeshi tangu tarehe 26 Julai, serikali yake ilipopinduliwa.
Burkina Faso yakifunga kituo cha redio kilichokosoa utawala wa Niger
Utawala wa kijeshi wa Burkina Faso umesitisha matangazo ya mojawapo ya kituo kikubwa cha redio nchini humo baada ya kurusha mahojiano yanayochukuliwa kuwa "matusi" kwa viongozi wa kijeshi wa Niger.
Redio Omega iliamuriwa kuacha mara moja kurusha matangazo yake siku ya Alkhamis (Agosti 10) hadi pale "patakapotolewa tangazo jengine", kwa mujibu wa tamko la Waziri wa Habari wa Burkina Faso, Rimtalba Jean Emmanuel Ouedraogo, aliyesema kuwa hatua hiyo ni "kwa maslahi mapana ya taifa."
Soma zaidi:ECOWAS waamua kujizuia kuingilia kati kijeshi Niger
Kituo hicho ambacho ni sehemu ya shirika la utangazaji la Omega linalomilikiwa na mwandishi wa habari na waziri wa zamani wa mambo ya nje, Alpha Barry, kilisitisha matangazo yake muda mchache tu baada ya tamko hilo la serikali.
Kosa la kituo hicho lilikuwa ni kurusha mahojiano yake na Ousmane Abdoul Moumouni, msemaji wa kundi linaloendesha kampeni ya kumrejesha Rais Mohamed Bazoum madarakani nchini Niger.
"Moumouni alitoa kauli ya matusi kwa utawala mpya wa Niger. Jumuiya yake inaendesha kampeni ya wazi ya machafuko na vita dhidi ya taifa huru la Niger na wanataka kumrejesha Bazoum madarakani kwa njia zozote zile," alisema Ouedraogo.
Redio Omega ilisema siku ya Ijumaa kwamba ingelitumia njia zozote kupambana na amri ya kusitisha matangazo yake, ambayo ilisema ni "uvunjwaji wa sheria na mashambulizi yasiyokubalika dhidi ya uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari."
Vyanzo: AFP, AP