ECOWAS yaendelea na mipango ya kutuma jeshi Niger
11 Agosti 2023Mataifa ya Afrika Magharibi leo yameendelea na mipango ya uwezekano wa kuivamia kijeshi Niger, ingawa bado wana matumaini ya mzozo uliopo kutatuliwa kwa njia ya amani.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, jana iliamuru kuundwa kwa kikosi cha dharura ili kurejesha utaratibu wa kikatiba.
ECOWAS imesema inataka demokrasia irejeshwe kwa amani, lakini njia zote ikiwa ni pamoja na za kijeshi zinawezekana.
Uongozi wa kijeshi wa Niger umesema utailinda nchi hiyo dhidi ya uingiliaji wowote wa kigeni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema nchi yake inaunga mkono juhudi zote zinazochukuliwa na ECOWAS kuhusu Niger.
Wakati huo huo, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amekosoa hali mbaya aliyonayo rais aliyepinduliwa Mohamed Bazoum na ametoa wito wa kuachiwa huru mara moja.