Ecowas yakamilisha mpango wa Mali
12 Novemba 2012Makubaliano hayo ni sehemu ya mpango utakaowasilishwa kwa Umoja wa Mataifa ili uidhinishwe ifikapo mwishoni mwa mwezi huu. Rais wa Cote d' Voire Alassane Outtara ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, amezitaja nchi zitakazochangia vikosi hivyo kuwa ni pamoja na Nigeria, Niger na Burkina Faso, lakini nchi nyingine za Afrika Magharibi na nyingine mbili au tatu zisizo za Afrika zinaweza kuchangia. Alisema wanajeshi hao watapelekwa mara moja baada ya Umoja wa Mataifa kuidhinisha mpango huo, ulioandaliwa na wataalamu wa kijeshi kutoka Afrika, Umoja wa Mataifa na Ulaya katika mji mkuu wa Mali, Bamako wiki iliyopita.
Mpango kutekelezwa kwa awamu
Mpango huo utatekelezwa katika kipindi cha miezi sita ukiwa na awamu ya maandalizi kwa ajili ya mafunzo na uanzishwaji wa vituo Mali kusini, ukifuatiwa na operesheni za kijeshi kaskazini. ECOWAS ilikamilisha muswada wa hivi karibuni siku ya Jumapili, lakini ilisema bado ina matumaini ya kuepusha mgogoro kupitia majadiliano. Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari baada ya mkutano huo katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, ilisema jumuiya hiyo inarejea matumaini yake kuwa majadiliano ndiyo njia bora.
Lakini iliongeza kuwa matumizi ya nguvu hayataepukika ili kusambaratisha kabisa mitandao ya kigaidi na ya uhalifu unaovuka mipaka ambayo inatishia amani na usalama wa kimataifa. Akizungumzia mpango huo, rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo alisema:
"Mpango huu unakwenda sambamba na azimio la Umoja wa Mataifa linaloidhinisha matumizi ya nguvu, kuwaondosha waasi na watawala huria ambao wameigeuza sehemu ya nchi hiyo kuwa isiyofuata sheria. Hili lazima tulifanye ili kuepusha madhara si tu kwa Mali, bali pia kwa kanda nzima na Afrika kwa ujumla."
Wanadiplomasia wasema operesheni itachukua muda mrefu
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliwapa viongozi wa Afrika siku 45 kuanzia Oktoba 12 mwaka huu kuandaa mpango wa kuingilia kati kijeshi ili kurejesha eneo la Mali kaskazini, lakini wanadiplomasia wanasema operesheni kama hiyo itachukua miezi mingi kukamilishwa. Algeria ambayo inatizamwa kama nchi muhimu kwa operesheni yoyote ya kijeshi, imekuwa ikisita kujihusisha, ikipendelea zaidi mazungumzo.
Licha ya kutokuwa mwanachama wa ECOWAS, Algeria ni muhimu kutokana na uwezo wake wa kijeshi, kijasusi, na uzoefu wake katika kupambana na wanamgambo wa kiislamu, pamoja na mpaka mrefu baina ya nchi hiyo na Mali. Wawakilishi kutoka nchi zilizoko nje ya ECOWAS walialikwa katika mkutano wa Jumapili, wakiwemo kutoka Mauritania na Algeria, na Afrika Kusini na Morocco ambazo zina viti katika baraza la usalama la umoja wa Mataifa. Libya na Chad pia ziliwakilishwa.
Wajumbe kutoka kundi la Kiislamu la Ansar Dine wanafanya mazungumzo na mpatanishi wa kanda, rais wa Burkina Faso Blaise Campaore, na wanachama wa kundi la waasi wa Tuareg, MNLA, wametaka kushiriki juhudi la kutatua mgogoro huo.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Josephat Nyiro Charo.