1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Edathy ataka kusafisha jina lake

17 Februari 2014

Aliyekuwa mbunge wa chama cha Social Democrats (SPD), Sebastian Edathy, ambaye anakabiliwa na kashfa ya kukutikana na picha za ngono za watoto, anataka kuchukua hatua za kujisafishia jina lake mahakamani.

https://p.dw.com/p/1BAFh
Mbunge wa zamani wa SPD, Sebastian Edathy.
Mbunge wa zamani wa SPD, Sebastian Edathy.Picha: picture-alliance/dpa

"Mimi sikuwa na picha za ngono. Nimechoka na kukashifiwa huku, maana ni kinyume na dhana ya kwamba mtu anakuwa hana makosa hadi pale mahakama inapomtia hatiani." Anasema Edathy, akinukuliwa na gazeti la Süddeutsche, baada ya wapelelezi kuendesha msako kwenye makaazi na ofisi zake. Na sasa anataka apande mahakamani kusafishwa jina lake. Mbunge huyo wa zamani sasa anataka kufungua malalamiko ya kuvunjiwa heshima, maana anaamini amekuwa akionewa kwa tuhuma hizi.

Mgogoro huu unatishia hata utendaji kazi wa serikali ya mseto wa vyama vya kihafidhina CDU/CSU na SPD anachotoka Edathy. Mkuu wa CSU, Gerda Hasselfeldt, anasema lazima SPD itowe maelezo ya kina juu ya hili, maana kilichopo sasa ni mgogoro wa imani na kuaminiana baina ya washirika hao kwenye serikali kuu ya shirikisho.

FDP yatiwa moyo ya Marekani

Mhariri wa Osnabrücker Zeitung anazungumzia mtazamo mpya wa chama cha kiliberali cha FDP, kuelekea mahusiano ya Ulaya na Marekani, ambacho kinaamini kuwa sasa Marekani iko tayari kushirikiana na Umoja wa Ulaya kwenye biashara huru kati yao, baada ya miaka kadhaa ya kusitasita. Mbunge wa Bunge la Ulaya kutokea FDP, Michael Theurer, anasema sasa ni Umoja wa Ulaya ndio unaopaswa kufungua milango na kuwa wazi zaidi.

Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Theurer, ambaye pia ni mwenyekiti wa FDP kwenye mkoa wa Baden-Württemberg, anaona kuwa mtazamo wa kiviwanda wa Ulaya sasa una soko kubwa nchini Marekani, litakalowafaidisha wafanyakazi na wajasiriamali wa Kijerumani. Muhimu tu ni kutekelezwa kikamilifu kwa makubaliano ya Julai mwaka jana, yaliyoanzisha eneo kubwa kabisa la biashara huria duniani, maarufu kama "Ushirikiano wa Biashara wa Bahari ya Atantiki."

Polisi yakosa wataalamu

Mhariri wa Mitteldeutsche Zeitung anazungumzia upungufu wa wataalamu kwenye jeshi la polisi, ambao sasa umevifanya vyama vya wafanyakazi kwenye jeshi hilo kuanza kupiga kelele.

Polisi nchini Ujerumani.
Polisi nchini Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa

"Miaka kumi ijayo tutakuwa tumeelemewa," ananukuliwa mkuu wa Umoja wa Wafanyakazi wa Polisi, Uwe Petermann. Dalili zipo. Maombi ya wanaojiunga na vyuo vya polisi yamepungua sana. Walioomba kujiunga mwaka jana walikuwa 3,014, asilimia 15 pungufu ya wale walioomba mwaka juzi, na ikiwa idadi ya chini kabisa ndani ya kipindi cha miaka 10.

Miongoni mwa sababu ni kupandishwa kwa viwango vya kufaulu kwa waombaji na sasa kuna upungufu mkubwa kwa vijana wanaomaliza masomo yao kujiunga na upolisi.

Mwandishi: Mohammed Khelef
Vyanzo: Süddeutsche Zeitung, Osnerbrücker Zeitung, Mitteldeutsche Zeitung
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman