Edna Adan Ismail kutoka Somaliland ashinda tuzo ya Templeton
16 Mei 2023Ameshinda tuzo hiyo kutokana na mapambano yake dhidi ya ukeketaji wa wasichana Afrika Mashariki na kutetea afya ya kina mama.
Edna Adan Ismail mwenye umri wa miaka 85, ni nesi mkunga, muasisi wa hospitali, mwanaharakati wa masuala ya afya na ambaye kwa miongo mingi amekuwa akipigania uimarishaji wa afya ya wasichana na wanawake kanda ya Afrika Mashariki.
Na kama ilivyo chanda chema huvishwa pete, mnamo Jumanne, alitangazwa mshindi wa tuzo ya Templeton mwaka 2023, ambayo ni kati ya tuzo kubwa zaidi ulimwenguni ambazo hutolewa kila mwaka kwa mtu binafsi.
Imani yake ikiwa imejengwa kwenye mizizi ya dini ya Uislamu, tuzo ya Tempelton inatambua juhudi za Bi Ismail kutumia sayansi kuthibitisha heshima ya wanawake na kuwasaidia kuimarika, kimwili na kiimani.
Bi Ismail ni mwanamke wa kwanza wa kiafrika kushinda tuzo hiyo
Heather Templeton Dill, rais wa Wakfu wa John Templeton unaosimamia tuzo hiyo, amesema Ismail ambaye amekuwa mwanamke wa kwanza wa Kiafrika kuishinda tuzo hiyo, ametumia mafundisho yake ya dini, familia na sayansi kuimarisha afya na mambo mengine yanayowahusu wasichana na wanawake walioko katika hatari.
"Ametumia sifa zake nyingi kupambana vikali dhidi ya ukeketaji wa wasichana na wanawake na kueleza kwamba hakika kadhia hiyo ni kinyume na mafundisho ya Uislamu, na huwasababishia wanawake madhara".
Ismail aliliambia shirika la Habari la Associated Press kwamba juhudi zinapaswa kuelekezwa kuzuia ugonjwa badala ya kuwatumbukiza watoto kwenye maumivu na madhara ya ukeketaji.
Ukeketaji wa wasichana na wanawake ungali tatizo katika baadhi ya jamii
Japo hatua zimepigwa, bado ukeketaji ni tatizo katika baadhi ya nchi. Juhudi zake za kupambana na tohara ya wasichana zinaendelea kupitia utetezi wake kimataifa na kwenye hospitali yake.
Ismail alisema atatenga kiasi cha fedha za tuzo hiyo kuipa hospitali ya Friends of Edna Maternity kununua vifaa vipya, kuwaajiri washauri na kutoa mafunzo kwa kizazi kipya cha wahudumu wa afya wanaohitajika zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki.
Ismail alizaliwa mwaka 1937 Hargeisa, mji mkuu wa iliyokuwa koloni la Uingereza Somaliland. Alisomea uuguzi na ukunga nchini Uingereza.
Baada ya masomo alirejea nchini mwake kuwahudumia raia wenzake. Kulingana na tangazo la ushindi wake, yeye ndiye alikuwa mwanamke wa kwanza kuendesha gari nchini mwake na pia mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa wizara ya Afya.
Miradi yake katika sekta ya afya Somaliland
Alikuwa na nia ya kujenga hospitali, akauza baadhi ya vitu vyake na pia kuchangisha fedha kote ulimwenguni na kufanikiwa. Hospitali ya Edna Adan Maternity ilifunguliwa mwaka 2002.
Wakati mfumo wa afya wa Somaliland ulipokuwa taabani, hospitali yake ilipiga hatua kubwa na kupunguza idadi ya vifo vya kina mama kutokana na uzazi.
Mradi wake wa elimu umetoa mafunzo kwa zaidi ya wanafunzi 4,000 ambao sasa ni madaktari, wauguzi na wataalam wengine katika sekta ya afya.
Zaidi ya watoto 30,000 wamezaliwa katika hospitali yake ambapo asilimia 80 ya wafanyakazi na 70% ya wanafunzi ni wanawake.
Tuzo ya Templeton inayokadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 1.4 ilianzishwa mwaka 1973 na mfadhili Sir John Templeton. Tuzo hiyo hutolewa kwa wale wanaotumia sayansi kutatua matatizo ya kijamii ulimwenguni.
Miongoni mwa waliowahi kushinda tuzo ya Templeton ni pamoja na marehemu Mama Teresa na hayati Askofu Desmond Tutu.
(Chanzo: APE)