El-Salvador yaandamwa na visa vya mauaji
27 Machi 2022Rais wa El Salvador Nayib Bukele amewatolea mwito wabunge kutangaza hali ya tahadhari nchini baada ya mamlaka za nchi kuwakamata viongozi wa juu wa magenge ya uhalifu nchini humo kufuatia wimbi la uwamgikaji damu lililosababisha watu chungunzima kuuwawa katika kipindi cha siku mbili tu.
Vurugu zinazofanywa na magenge ya uhalifu nchini humo zimeongezeka ambapo polisi imeripoti kwamba watu 62 waliuwawa jana Jumamosi peke yake.
Jeshi la polisi nchini humo liliandika kwenye ukurasa wa mtandao wa Tweeter kwamba halitorudi nyuma katika vita hivi dhidi ya magenge na wala halitopumzika hadi wahalifu waliohusika na matukio hayo watakapokamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Mauaji hayo yamefanyika katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo.Saa chache kabla ya mauaji polisi na jeshi liliwakamata viongozi chungunzima wa genge linalojulikana kama Mara Salvatrucha-MS-13 kuhusiana na matukio kadhaa ya mauaji.
Katika hatua za kukabiliana na ongezeko la vurugu rais wa Salvador Bukele ameliomba bunge ambalo linahodhiwa na chama chake kukutana na kutangaza hali ya dharura ambapo chini ya hali hiyo uhuru unaweza kudhibitiwa kwa kiasi fulani.
Katiba ya nchi hiyo inasema kwamba hali ya dharura inaweza kutangazwa pale panapotokea hali ya vita, uvamizi, uasi, uhaini, majanga, au maradhi yanayosababisha janga au matukio mengine makubwa au hali yoyote inayoweza kusababisha ukosefu mkubwa wa utulivu katika sheria za nchi.
Rais huyo alikutana kwa dharura maafisa wa ngazi za juu wa usalama pamoja na mwanasheria mkuu wa nchi kujadili hali iliyopo.
Wakili mkuu wa serikali kuhusu masuala ya haki za binadamu Ricardo Martinez ameutaka umma kuendelea kuwa watulivu na kuchangia kuunga mkono amani katika taifa hilo.
Mwaka Jana Novemba El Salvador ilikabiliwa na wimbi jingine la umwagikaji damu uliosababisha kiasi watu 45 kuuwawa katika kipindi cha siku tatu tu.
Genge linalojiita Mara Salvatrucha na Barrio -18 ni miongoni mwa magenge mengi mengine nchini humo na yana wanachama 70,000 katika ElSalvador kwa mujibu wa mamlaka za nchi na harakati zao ni pamoja na kuendesha mauaji, utesaji, ulanguzi wa madawa ya kulevya miongoni mwa uhalifu mwingine.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Iddi Ssessanga