130112 Sirleaf zweite Amtszeit
16 Januari 2012Ellen Johnson-Sirleaf alijinyakulia ushindi kama mchezo tu. Kwani katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais, alishinda asilimia 90.7 ya kura zilizopigwa. Lakini nchini humo pia kuna wengine waliovunjika moyo.
"Watu wengi wanahisi kuwa wametengwa na yale yanayotokea katika jamii. Kuna mengi yanayotarajiwa na umma katika miaka ijayo." Anasema rais wa umoja wa vyombo vya habari wa Liberia, Peter Quaqua.
Yeye anasema, matatizo ya sasa ni yale yaliyokuwepo tangu hapo zamani - kuanzia rushwa iliyokithiri kote nchini pamoja na matatizo ya sekta ya elimu na ukosefu mkubwa wa ajira. Watu wanahisi kuwa wao wala hawakufanikiwa kutoka na yale yaliyopatikana nchini humo. Kwa maoni ya Quaqua, sasa wakati umewadia kutekeleza ahadi zilizotolewa kwenye kampeni za uchaguzi.
Changamoto kubwa kabisa inayomkabili rais wa Liberia, ni kuwapatia watu ajira. Inatathminiwa kuwa idadi ya wakosa ajira nchini humo imefikia asilimia 80.
"Idadi kubwa ya vijana wasio na ajira na waliokosa elimu ni kama bomu linalongojea kuripuka. Ukweli huo ulidhihirika wakati wa uchaguzi." Anasema Mtaalamu wa masuala ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Massachusetts Boston, Michael Keating.
Mapambano makali yalizuka katika mji mkuu wa Liberia, Monrovia, muda mfupi tu baada ya uchaguzi. Watu wanne waliuawa katika machafuko hayo. Kwa upande mwingine, Rais Johnson-Sirleaf ameweza kutekeleza mambo kadhaa katika nchi hiyo yenye utajiri wa malighafi. Wakati wa awamu yake ya kwanza, kiongozi huyo alisifiwa kwa kufanikiwa kuwavutia wawekezaji nchini humo. Inatumainiwa kuwa mikataba iliyotiwa saini pamoja na makampuni makubwa ya kimataifa, itaingiza fedha nyingi nchini humo na itatoa nafasi mpya za ajira.
Lakini uwekezaji huo pia unakwenda sambamba na tatizo moja - rushwa. Hiyo ni changamoto inayoendelea kumkabili rais wa Liberia. Yeye aliahidi kukomesha rushwa wakati wa awamu yake ya kwanza madarakani. Lakini katika miaka sita iliyopita, hakuna hatua imara iliyochukuliwa, anasikitika Peter Quaqua.
Anasema, tatizo hilo linalojadiliwa sana, lakini wengi miongoni mwa wale waliohusika na rushwa wala hawakuadhibiwa. Kwa maoni yake watu hao wanapaswa kushtakiwa mahakamani, ama sivyo ahadi za kukomesha rushwa zitabakia maneno matupu.
Mwandishi: Stefanie Duckstein/ZPR
Tafsiri: Prema Martin
Mhariri: Sekione Kitojo