England na Scotland huenda zikaadhibiwa na FIFA
12 Novemba 2016England na Scotland zinakabiliwa na hali ya sintofahamu ya kusubiri kuona iwapo zitakabiliwa na vikwazo baada ya kuchukua hatua ya kufanya kumbukumbu ya maombolezi kwa watu waliofariki katika vita nchini Uingereza katika mchezo wao wa kufuzu kucheza katika kombe la dunia.
Timu hizo mbili, zikiongozwa na nahodha wa timu ya taifa ya England , Wayne Rooney na mwenzake wa Scotland Darren Fletcher , walivaa kitambaa cheusi mkononi pamoja na ua jekundu katika mchezo wao jana Ijumaa uwanjani Wembley, ambapo wenyeji walishinda kwa mabao 3-0.
Shirikisho la kandanda duniani FIFA limeonya hatua hiyo kuwa inaweza kukiuka sheria inayopiga marufuku "kauli mbiu za kisiasa, kidini ama za binafsi, taarifa , ama picha".
Akizungumza kabla ya mchezo huo , kocha wa mpito wa England Gareth Southgate alisema: "Tunafuraha kwamba tunaweza kuwaenzi watu waliojitoa muhanga kuitetea nchi yetu ambao wametangulia."
Watu nchini Uingereza kwa kawaida huvaa alama ya maua katika siku zinazoelekea Novemba 11, siku ya Armistice ilipotiwa saini mwishoni mwa vita vikuu vya kwanza vya dunia mwaka 1918, kuwakumbuka watu waliofariki nchini humo kutokana na vita hivyo.Vyama vya kandanda vya England na Scotland vinaweza kuadhibiwa kwa hatua za kinidhamu iwapo kamisaa wa mchezo huo kutoka FIFA atataja kuhusu vitambaa hivyo vya mkononi katika ripoti yake kuhusu mchezo huo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Sylvia Mwehozi