1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan aahidi ushirikiano na Urusi

Admin.WagnerD10 Agosti 2016

Rais Vladimir Putin wa Urusi na mwenzake wa Uturuki Recep Erdogan jana(09.08.2016) waliahidi kuimarisha uhusiano wao baada ya mkutano wao wa kwanza tangu Uturuki ilipoiangusha ndege ya Urusi Novemba mwaka jana.

https://p.dw.com/p/1JfSi
Russland Recep Tayyip Erdogan und Wladimir Putin in St. Petersburg
Rais Putin (kushoto na Recep Erdogan wa Uturuki (kulia)Picha: picture-alliance/dpa/A. Nikolsky

Uturuki wakati huo huo imeuonya Umoja wa Ulaya kwamba unafanya makosa makubwa katika mtazamo wake kuhusu jaribio lililoshindwa la mapinduzi nchini humo.

Erdogan alifanya ziara hiyo katika mji alikozaliwa rais Putin wa St. Petersburg ikiwa pia ya kwanza nje ya nchi yake tangu pale lilipofanyika jaribio lililoshindwa la mapinduzi dhidi yake mwezi uliopita ambalo lilizusha msako mkubwa dhidi ya wapinzani na kuweka kiwingu katika uhusiano kati ya Uturuki na mataifa ya magharibi.

Türkei Ausnahmezustand: Folgen des Putsches
Vifaru vya jeshi vikilinda doria nchini Uturuki baada ya jaribio la mapinduziPicha: Getty Images/C. McGrath

"Tulipitia katika wakati mgumu sana wa uhusiano wetu kati ya mataifa haya mawili na kwa kiasi kikubwa , na nahisi marafiki zetu wa Uturuki wanataka, kuweka kando matatizo hayo," Putin aliwaambia waandishi habari akiwa pamoja na Erdogan.

Erdogan kwa upande wake alionesha matumaini yake kwamba uhusiano huo utakuwa imara zaidi na kuonesha msisitizo wa vipi ilikuwa muhimu kwa Putin kuonesha uungaji wake mkono kwa Erdogan baada ya jaribio la mapinduzi.

Vikwazo dhidi ya Uturuki

Kuangushwa kwa ndege ya kijeshi ya Urusi na ndege ya kijeshi ya Uturuki chapa F-16 katika mpaka na Syria Novemba mwaka jana kulishuhudia Putin akiweka vikwazo dhidi ya Uturuki na kuzusha vita vya maneno ambavyo viliharibu uhusiano wao.

Türkei Symbolbild AKP Anhänger Nationalismus
Raia wa Uturuki wakionesha mshikamano baada ya jaribio la mapinduziPicha: Reuters/A. Konstantinidis

Lakini kwa mshituko mkubwa mwishoni mwa mwezi Juni , Putin alikubali barua kutoka kwa Erdogan inayoelezea masikitiko yake kuhusiana na tukio hilo na kuwa kama kuomba msamaha.

Putin aliondoa haraka marufuku ya mauzo ya vivutio kwa watu wanaotaka kutembelea Uturuki katika mapumziko, na kuashiria kwamba Urusi itafikisha mwisho hatua dhidi ya uagizaji wa vyakula kutoka Uturuki na makampuni ya ujenzi.

Türkei Istanbul Verhaftungen Soldaten Polizei Gewalt
Polisi wakupambana na ghasia wakimkamata mwanajeshi wa UturukiPicha: Getty Images/AFP/B.Kilic

Hofu ya mataifa ya magharibi

Hivi sasa kutokana na jaribio hilo la mapinduzi lililoshindwa Julai 15 , kuna hofu katika miji mikuu ya mataifa ya magharibi kwamba mwanachama wa NATO - Uturuki inaweza kujisogeza karibu zaidi na Urusi, ambapo Erdogan alionesha wazi kwamba anajihisi ameangushwa na Marekani na Umoja wa ulaya.

Katika mahijiano na shirika la habari la serikali la Anadolu nchini Uturuki , waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo Mevlut cavusoglu alisema:

Türkei Putschversuch Festnahmen
Kundi la wafanyakazi wa jeshi wakikamatwaPicha: picture-alliance/abaca

"Kukaribiana kati ya Uturuki na Urusi si ishara ya ujumbe kwa mataifa ya magharibi. Hata hivyo , iwapo mataifa hayo yataipoteza Uturuki itakuwa ni makosa yao wenyewe, na sio kutokana na mahusiano mazuri kati ya Uturuki na Urusi."

Wakati huo huo ujumbe wa maafisa wa wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki , ulinzi na ujasusi unakwenda Urusi kwa majadiliano ya kutafuta suluhisho katika mzozo wa Syria, imesema taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki leo.

Belgien Jens Stoltenberg NATO PK
Katibu mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: Reuters/F. Lenoir

Nalo shirika la NATO limesema leo kwamba uanachama wa Uturuki katika shirika hilo hauna mjadala na kwamba Ankara inaweza kulitegemea shirika hilo katika mshikamano wake na uungaji mkono baada ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwezi uliopita.

Mwandishi: Sekione Kitojo/rtre/afpe/dpae

Mhariri: Mohammed Khelef