1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan aapa kuijenga upya Uturuki baada ya tetemeko

15 Februari 2023

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameapa kuendelea na juhudi za uokozi ikiwa ni zaidi ya wiki moja baada ya tetemeko kubwa la ardhi kuitikisa nchi yake na nchi jirani Syria.

https://p.dw.com/p/4NUur
Türkei | Erdogan sprcht zur AKP
Picha: Mehmet Kaman/AA/picture alliance

 

Idadi jumla ya vifo nchini Uturuki na Syria imepanda hadi zaidi ya watu 41,000 na manusura wengi wanakabiliwa na baridi kali, baada ya kuwachwa bila makaazi kutokana na uharibifu mkubwa uliofanyika katika miji ya nchi hizo mbili.

Erdogan amesema wataendelea na kazi hadi watakapomuondoa raia wa mwisho aliyebaki kwenye majengo yaliyoporomoka. Amesema tathmini ya majengo, ambayo maelfu yaliharibiwa, itakamilika katika wiki moja na ujenzi mpya kuanza katika miezi kadhaa. 

UN:Watoto milioni 7 wameathirika kote Uturuki na Syria

Wakati huo huo, misafara zaidi ya Umoja wa Mataifa ilifaulu kuingia kaskazini magharibi mwa Syria ikiwa na bidhaa za msaada kwa waathirika wa tetemeko hilo la ardhi. Hii ni baada ya vivuko vya mpakani kufunguliwa. Idadi ya waliokufa Uturuki ni 35,418, wakati nchini Syria ni zaidi ya watu 5,814 waliokufa.