Erdogan aonya kuendeleza operesheni makubaliano yakikiukwa
18 Oktoba 2019Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema nchi yake itaendelea na uvamizi wake kaskazini mwa Syria kwa kasi kuliko awali ikiwa makubaliano na Marekani ya kusitisha operesheni na kuruhusu vikosi vya Kikurdi kuondoka hayatatekelezwa kikamilifu.
Erdogan aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Ankara amesema Uturuki haitakuwa na shida yoyote ikiwa majeshi ya Syria yanayoungwa mkono na Urusi yataingia katika maeneo ambayo wanamgambo wa Kikurdi wa kundi la YPG wametimuliwa, huku akiongeza kuwa Uturuki haina lengo la kusalia katika maeneo chini ya udhibiti wake, kaskazini mwa Syria.
Kuhusu barua ya rais wa Marekani Donald Trump kwake ambapo Trump alimwambia Erdogan asiwe mpumbavu na anayejiona kuwa na nguvu, Erdogan amesema alimtaarifu kwa njia ya simu Rais Trump kuhusu operesheni yake, siku moja kabla ya kuianza. Na hivyo kile kinachohitajika kitatekelezwa muda wake kamili ukiwadia.
''Mojawapo ya makubaliano yetu na Marekani ni kwamba vikosi vyetu vya usalama, havitaondoka kutoka eneo hilo. Wanajeshi wetu wataendelea kuwa pale kuona kama kweli vikosi vya Kikurdi hakika vinaondoka eneo hilo au la.'' Amesema Erdogan.
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk amesema kile kinachoitwa kuwa makubaliano ya kusitisa mashambulizi Syria ni sawa na kuwalazimisha Wakurdi kusalimu amri. Tusk ameitaka Uturuki kusitisha mara moja operesheni yake kaskazini mashariki mwa Syria.
Baada ya nchi za Umoja wa Ulaya kuishutumu Uturuki kwa uvamizi wake Syria, Tusk amesema makubaliano kati ya Marekani na Uturuki kuacha mashambulizi kwa siku tano si mpango mzito.
Tusk aliyezungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya, amesema hilo silo lile walilolitarajia na amesema wanasisitiza wito wao kuitaka Uturuki kuachana na shughuli zake za kijeshi nchini Syra mara moja na iyaondoe majeshi yake kwa kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.
Hayo yakijiri, vyanzo vya habari vya Kikurdi pamoja na kundi moja linalofuatilia haki za binadamu hiyo limesema mashambulizi yameendelea leo kaskazini mashariki mwa Syria, siku moja baada ya Marekani na Uturuki kufikia makubaliano ya kusitisha mashambulizi eneo hilo.
Kundi linalofuatilia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake makuu Uingereza limesema mashambulizi yamesikika katika mpaka wa mji wa Ras al-Ain, japo kuna utulivu katika maeneo mengine.
Kundi hilo limeongeza kuwa machafuko katika eneo hilo yametokea kati ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Uturuki na wapiganaji wa Kikurdi, licha ya makubaliano ya usitishwaji mashambulizi.
Vyanzo vya habari vya Kikurdi vimelieleza shirika la habari la hapa Ujerumani DPA kuwa mashambulizi ambayo yamefanywa na Uturuki yamelenga Ras al-Ain na kwamba hospitali ambapo wengi wa majeruhi wanatibiwa imeshambuliwa.
Shirika la haki za binadamu linalofuatilia hali nchini Syria, limesema wakati wa ghasia hizo, waasi wanaoungwa mkono na Uturuki waliuzuia msafara wa Hilal Nyekundu wa Wakurdi, kuingia katika mji huo ili kuwaondoa majeruhi. Shirika hilo limeongeza kuwa mashambulizi madogo madogo pia yametokea mji wa Ain Issa
Wanamgambo wa Kikurdi wa kundi la SDF wameilaumu Uturuki kwa kushambulia maeneo ya raia na kukiuka makubaliano ya usitishwaji mashambulizi kwa siku tano.
Msemaji wa SDF Mustafa Bali amesema licha ya makubaliano hayo, ndege za kivita za Uturuki na magari ya kivita yameendelea kushambulia maeneo ya wapiganaji wao na hata maeneo ya raia.
Hapo jana, makamu wa rais wa Marekani Mike Pence alisema Uturuki itasitisha mashambulizi kwa muda wa saa 120 ili kuruhusu wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria kujiondoa katika maeneo salama.
Vyanzo: DPAE, RTRE, APE