1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan asaka ufumbuzi wa mgogoro wa ghuba

23 Julai 2017

Uturuki yapania kuupatia ufumbuzi wa haraka mvutano wa kidiplomasia kati ya Qatar na nchi nne za kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia

https://p.dw.com/p/2h1QZ
Türkei Präsident Recep Tayyip Erdogan und seine Frau fliegen nach Saudi-Arabien ab
Picha: picture-alliance/abaca/Y. Bulbul

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan yuko  eneo la ghuba nchini Saudi Arabia  kwa ziara muhimu inayolenga kuutafutia ufumbuzi mvutano baina ya mshirika wake Qatar na nchi nne za kiarabu, Saudi Arabia, Bahrain, Umoja wa Falme za kiarabu na Misri. Tayari rais Erdogan amesema hakuna mtu yoyote anayepata faida kwa kuuendeleza mgogoro huo. Katika ziara yake hiyo rais huyo wa Uturuki kwanza anakutana na uongozi wa Saudi Arabia mjini Jeddah kabla ya kuelekea Kuwait ambayo ni mpatanishi katika mgogoro huu na baadaye kuelekea Qatar kesho Jumatatu ambako kwa mara ya kwanza atakutana katika mazungumzo ya ana kwa ana na mfalme Tamim bin Hamad al-Thani wa Qatar tangu kuzuka kwa mvutano huo.

Akiwa katika uwanja wa ndege wa Istanbul kabla ya kuondoka kuanza safari yake hiyo rais Erdogan aliwatuhumu maadui kwamba wanataka kuuchochea zaidi mvutano na kuzusha hali ya wasiwasi baina ya ndugu katika kanda hiyo.Kadhalika rais huyo ameisifu Qatar kwa kuonesha tabia njema katika mgogoro huu akisema ni nchi iliyoamua kufuata njia ya mazungumzo kuupatia ufumbuzi mgogoro huo. Uturuki inamatumaini kwamba ziara hii itasaidia kuleta mafanikio katika kanda hiyo.

Kronprinz Mohammed bin Salman
Picha: picture-alliance/AP Photo/Saudi Press Agency

Mvutano baina ya nchi hizo za Ghuba ulianza tarehe 5 mwezi Juni ambapo Saubi Arabia, Bahrain, Umoja wa Falme za kiarabu na Misri ziliamua kukata uhusiano wao na Qatar kwa kuituhumu nchi hiyo kwamba inawaunga mkono watu wenye itikadi kali na kwamba inashirikiana kwa karibu zaidi na Iran taifa ambalo ni la kishia.Hata hivyo utawala wa kifalme mjini doha unakanusha tuhuma hizo na imekuwa ikungwa mkono kwa dhati na Uturuki katika kipindi chote cha mgogoro.Huu ni mgogoro ambao umeiweka Uturuki katika nafasi ngumu na rais Erdogan ameshasema mara kwadhaa kwamba anataka kuhakikisha mgogoro huu umamaliza haraka iwezekanavyo.

Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita Qatar imeonekana kuwa mshirika namba moja wa Uturuki katika eneo la Mashariki ya Kati huku nchi hiyo ya Uturuki na serikali ya mjini Doha zikishirikiana kwa karibu katika masuala kadhaa ikiwemo mgogoro wa Syria ambapo nchi zote mbili ni maadui wa rais Bashar al Assad.Uturuki iko katika harakati kabambe za kuweka kambi ya kijeshi nchini Qatar ikiwa ni kambi pekee a nchi hiyo katika kanda hiyo na harakati hizo za Uturuki zimeongezeka kasi tangu ulipozuka mvutano huu na inaripoti kwamba kufikia hivi sasa kuna wanajeshi 150 wa Uturuki katika kambi hiyo.

Katar - Scheich Tamim bin Hamad Al Thani
Mfalme wa Qatar Tamim bin Hamad al ThaniPicha: picture alliance/AA/Qatar Emirate Council

Rais Ergogan anasema tangu mwanzo wa mgogoro huu wa Qatar nchi yake imekuwa ikizingatia zaidi upande wa amani,uthabiti,mshikamano na mdahalo.Pamoja na yote hayo Uturuki ambayo inapitia kipindi cha msukosuko na Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani pia haitaki kusababisha hali ya kuvutana katika uhusiano wake na Saudi Arabia ambayo ndio nchi yenye usemi katika kanda hiyo ya ghuba ya kiarabu.Tangu kuanza kwa mgogoro huu Uturuki imeshapeleka ndege 200 za mizigo zikiwa zimesheheni msaada wa kibinadamu nchini Qatar.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:John Juma

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW