1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan kuiongoza Uturuki tena

25 Juni 2018

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amepata ushindi katika uchaguzi wa rais unaompa fursa ya kuongoza kwa miaka mingine mitano, huku akiwa na mamlaka makubwa.

https://p.dw.com/p/30DJb
Wahlen Türkei - Erdogan erklärt sich zum Sieger
Picha: picture alliance/AP Photo/L. Pitarakis

Upinzani hata hivyo umezusha maswali makali kuhusiana na namna uchaguzi huo ulivyoendeshwa.

Erdogan ambaye ameitawala Uturuki kwa miaka 15 iliyopita alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais bila kuhitaji duru ya pili na akauongoza muungano wa chama chake tawala kwa kupata wingi wa viti bungeni.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 64, ambaye ushindi huo ulikuwa mkubwa kuliko ilivyotabiriwa na wachambuzi wengi, ameapa kutekeleza haraka mfumo mpya wa rais aliye na madaraka mengi ulioidhinishwa katika kura ya maoni ya Aprili 2017 ambao wapinzani wanahofia kuwa utamfanya kuongoza kwa mkono wa chuma.

Erdogan alipata asilimia kubwa ya kura za Waturuki wanaoishi Ujerumani kuliko nchini Uturuki kwenyewe. Wafuasi wake wamesherehekea katika mitaa ya Berlin mapema leo wakipeperusha bendera za Uturuki na chama cha AKP huku wakilitaja jina la Rais huyo wakisema kwamba ni kiongozi wao. Lakini sherehe hizo hazijapokelewa vyema na kila mmoja.

Cem Özdemir ailaani tabia ya wafuasi wa Erdogan Ujerumani

Kulingana na hesabu ya asilimia 80 ya kura za jamii ya Waturuki walioko Ujerumani asilimia 65.7 walimpigia kura Erdogan na ni jambo lililozua shangwe kwenye mitaa ya Mji Mkuu wa Ujerumani Berlin baada ya Erdogan kutangazwa mshindi.

Wahlen Türkei - Erdogan erklärt sich zum Sieger
Rais wa Uturuki Erdogan akiwa na mkewe Emine ErdoganPicha: picture-alliance/AA/M. Kaynak

Mbunge wa Ujerumani Cem Özdemir ambaye pia ni kiongozi mwenza wa zamani wa chama cha Kijani na ambaye familia yake inatokea Uturuki ameilaani tabia hiyo ya wafuasi wa Erdogan Ujerumani akisema ni jambo linalostahili kumtia hofu kila mmoja. Özdemir ameliambia shirika la habari la Ujerumani DPA, "hawasherehekei tu ushindi wa dikteta wao bali wanaonyesha kuikataa demokrasia yetu wakati huo huo," alisema mbunge huyo.

Mwenyekiti wa jamii ya Waturuki nchini Ujerumani Gokay Sofuoglu amesema huo uungwaji mkono mkubwa wa Erdogan unaoonyeshwa na wafuasi wake unaweza kuwa ulianzia enzi za wahamiaji waliotoka Uturuki na kuingia Ujerumani katika miaka ya 1960 kusaidia katika ujenzi wa nchi baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Sofuoglu amesema idadi kubwa ya wahamiaji hao walitokea katika maeneo ya wahafidhina na walikuwa hawajali haki za binadamu.

Mwenyekiti huyo amesema "kulingana na wao, Erdogan ndiye aliyejenga hospitali, barabara na maduka," alisema Gokay.

Uturuki inatawaliwa kwa misingi ya demokrasia

Huku hayo yakijiri Rais wa Urusi Vladimir Putin Jumatatu alimpongeza Rais Erdogan kwa kuchaguliwa kwake kwa mara ya pili, akisema matokeo ya kura yanaonyesha ushawishi mkubwa wa kisiasa na uungwaji mkono mkubwa alio nao kiongozi huyo. Putin alisisitiza hii ni ishara ya imani ya wafuasi wake kwenye uongozi wake katika kuyatafutia suluhu masuala ya matatizo ya kijamii na kiuchumi yanayoikabili nchi hiyo ili kuiongezea nguvu nafasi yake kimataifa. 

Wahlen Türkei - Erdogan erklärt sich zum Sieger - Erdogans Anhänger feiern
Wafuasi wa Erdogan wakisherehekea ushindi wakePicha: picture alliance/AA/M. Dermencioglu

Erdogan mwenyewe amesema kwamba ushindi wake umeonyesha kwamba Uturuki ni nchi inayoendeshwa kwa misingi ya demokrasia, "mshindi wa huu uchaguzi ni demokrasia, taifa letu. Washindi wa uchaguzi huu ni kila mmoja ya raia milioni 81 wa Uturuki," alisema kiongozi huyo. "Nawashukuru nyote muliokwenda kupiga kura leo katika sherehe hii ya demokrasia, ambayo ina idadi kubwa ya waliojitokeza kupiga kura katika historia yetu," aliongeza Rais Erdogan.

Uchaguzi huo wa Uturuki unaukaribisha mfumo mpya wa utawala nchini humo ambapo cheo cha Waziri Mkuu kimefutiliwa mbali sasa na Rais ndiye atakayekuwa kiongozi wa nchi na serikali. Kwa mara ya kwanza nchini Uturuki, upinzani uliokuwa umeungana ulimpa kitisho cha kumuondoa madarakani Rais Erdogan.

Mwandishi: Jacob Safari/DPAE/AFPE

Mhariri: Caro Robi