1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan na Putin wakutana Sotchi

Oumilkheir Hamidou
22 Oktoba 2019

Mkutano kati ya rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na mwenzake wa Urusi mjini Sotchi, kasheshe ya Brexit na tathmini ya nusu mhula ya shughuli za serikali kuu ya muungano mjini Berlin magazetini

https://p.dw.com/p/3RhMi
Türkei Erdogan auf der Reise nach Sotschi
Picha: picture-alliance/AA/M. Ali Ozcan

Tunaanza na juhudi za kujongeleana Uturuki na Urusi. Viongozi wa nchi hizo mbili, rais Vladimir Putin wa Urusi na Erdogan wa Uturuki wanatarajiwa kukutana  katika mji wa Sotchi. Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linamulika uhusiano huo na kuandika: "Tangu wiki kadhaa sasa Recep Tayyip Erdogan amekuwa akizidhihaki mtindo mmoja nchi za magharibi. Barua ya onyo kutoka kwa rais wa Marekani aliyemtaka "aache upumbavu" na awatendee ipasavyo wakurd", ameitupa ndani ya debe la taka. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani amemtaja kuwa ni mwenye kuhitaji "kujifunza zaidi". Lakini leo hakuna mzaha, leo Erdogan anakutana na Vladimir Putin huko Sotchi. Hakuna yeyote anaemfanyia dhihaka rais wa Urusi. Putin amepata nguvu kupita wakati wowote ule mwengine. Urusi inaidhibiti Syria , na sio tu angani. Vikosi vya Putin vinakutikana hivi sasa takriban katika maeneo yote ya Syria na wao ndio pekee yao wanaolinda utulivu nchini humo."

Waziri mkuu wa Uingereza apimana nguvu na bunge la nchi yake

Kasheshe ya Brexit haina mwisho. Jana spika wa bunge John Bercow amepinga shauri la waziri mkuu la kuyapigia kura makubaliano yaliyofikiwa pamoja na Umoja wa ulaya. Gazeti la "Weser Kurier" linamulika kizungumkuti cha Brexit na kuandika: "Kinyume na katika utawala wa muda mfupi wa Theresa May, hivi sasa  maamuzi ya wawakilishi wa wananchi wa Uingereza si ya uharibifu. Wanataka kuhakikisha njia zote za kisheria zinafuatwa ili kuepukana na balaa la kujitoa katika Umoja wa ulaya bila ya maridhiano. Na hilo bila ya shaka ni kwa masilahi ya Umoja wa ulaya pia. Matokeo yake ni kwamba vionmgozi walioko mjini Brussels watabidi wawre na subira."

Serikali kuu  ya Ujerumani yastahili sifa

Mada yetu ya mwisho magazetini inamulika kwa jinsi gani serikali kuu ya Ujerumani imetekeleza au la ahadi ilizotoa, nusu njia tangu ilipoingia madarakani. Gazeti la Märkische Oderzeitung linaandika: "Watu wangetegemea majisifu makubwa zaidi kutoka tume ya kutathmini shughuli za serikali kuu ya muungano, seuze tena wakfu wa Bertelsman ulikwisha toa ripoti yake wiki kadhaa kabla na kusema "serikali kuu ya muungano ina stahiki sifa  zaidi kwakuwa majukumu iliyojiwekea imeyatekeleza ipasavyo.Kwamba ujumbe huo haujawafikia wakusudiwa, hilo si kosa la vyombo vya habari."