1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan: Viongozi wa Ulaya ni waongo

26 Julai 2016

Erdogan amesema Viongozi wa Ulaya sio wa kweli na hasa kutokana na kushindwa kutimiza ahadi yao katika makubaliano waliyofikia pamoja juu ya suala la kuwazuia wahamiaji kuingia barani Ulaya

https://p.dw.com/p/1JVvI
Rais Erdogan akihojiwa na mwandishi wa kituo cha TV cha ARD
Rais Erdogan akihojiwa na mwandishi wa kituo cha TV cha ARDPicha: picture-alliance/AA/K. Ozer

Recepp Tayyip Erdogan alihojiwa na kituo cha Televisheni ya umma ya Ujerumani ARD na mahojiano hayo kurushwa hewani jana usiku,kwa kauli yake kiongozi huyo wa Uturuki amewaita viongozi wa Ulaya kuwa watu wasiokuwa wakweli kwa kuwa wameshindwa kutimza ahadi waliyotoa kwa nchi yake baada ya kufikia makubaliano kuhusu suala la kuwazuia wahamiaji kuingia Ulaya.Amesema Umoja wa Ulaya ulituma Yuro milioni 2 tu kati ya Yuro bilioni tatu ulizoahidi kuipatia Uturuki kama ilivyokubaliwa katika mkataba wa pamoja ulioitaka Uturuki badala yake ikubali kurudishiwa wakimbizi walioingia Ulaya

Kadhalika Erdogan amewakosoa viongozi wa Ulaya kwa kushindwa vile vile kutimiza ahadi ya kuondoa sharti la visa kwa raia wa Uturuki wanaotaka kusaifiri kuingia Ulaya. Sambamba na hayo Erdogan ameitetea adhabu ya kifo kwa kusema jaribio la serikali yake kurudisha adhabu hiyo kali duniani limetokana na matakwa na mwito wa wananchi wa taifa lake na kwamba adhabu hiyo imekuwepo takriban kila mahala ispokuwa barani Ulaya.

Wafuasi wa Erdogan wakiwa mjini Ankara
Wafuasi wa Erdogan wakiwa mjini AnkaraPicha: DW/D. Cupolo

Hata hivyo wadadisi wa mambo nchini Ujerumani wanasema mahojiano aliyofanyiwa Erdogan na kituo hicho chaTelevisheni ya Umma nchini Ujerumani imempa nafasi rais huyo ya kujitangaza baada ya jaribio la serikali yake kupinduliwa na zaidi wafuasi wake nchini Ujerumani watakuwa wamefurahishwa na jinsi ambavyo rais huyo ameweza kujitangaza ipasavyo.Hata hivyo bado serikali ya Erdogan inaendeleza kamatakamata kufuatia jaribio la mapinduzi na inaarifiwa majenerali wawili wanaohudumu nchini Afghanistan wamekamatwa Dubai wakituhumiwa kuhusika na mapinduzi hayo yaliyoshindwa ya mwezi Julai dhidi ya rais Erdogan.

Meja jenerali Mehmet Cahit Bakir ambaye ni kamanda ni kikosi kazi cha Uturuki nchini Afghanistan na Brigedia Jenerali Sener Topuc walikamatwa katika uwanja wa ndege wa Dubai kufuatia ushikiriano wa idara za kijaasusi za Uturuki na maafisa wa Umoja wa Falme za kiarabu.

Rais Recep Erdogan na Waziri mkuu Binali Yildirim Akar na mkuu wa majeshi Hulusi Akar
Rais Recep Erdogan na Waziri mkuu Binali Yildirim Akar na mkuu wa majeshi Hulusi AkarPicha: picture-alliance/dpa/Turkish President Press Office

Kando na hayo Uturuki inajongeleana hivi sasa na Urusi ambapo leo hii ujumbe wa Urusi umekuwa na mazungumzo na Uturuki juu ya kuanzisha tena mradi unaolenga ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Urusi kwenda Uturuki.Naibu waziri mkuu wa Urusi Arkady Dvorkovich na mwenzake wa Uturuki Mehmet Simsek wawalikutana mapema hii leo na kuuzungumzia juu ya kuwepo dhamira ya kurudisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga