1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia, Eritrea waanzisha mashambulizi mapya Tigray

1 Septemba 2022

Vikosi vya waasi katika katika jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia vimesema, wanajeshi wa vikosi vya usalama vya Ethiopia na Eritrea wameanzisha mashambulizi makubwa ya pamoja dhidi yao.

https://p.dw.com/p/4GImK
Tigray-Krise in Äthiopien
Picha: Eduardo Soteras/AFP

Msemaji wa vikosi vya TPLF amesema wanajeshi wa Ethiopia wameanzisha mashambulizi hayo ili kuwaua na kuwaumiz watu wa Tigray. 

Msemaji wa Chama cha ukombozi cha watu wa Tigray, TPLF, Getachew Reda ameandika kupitia ukurasa wa twitter kwamba majeshi ya Ethiopia na Eritrea yameanzisha mashambulizi hayo makubwa mapema hii leo katika eneo la Adyabo, kaskazinimagharibi mwa Tigray.

Shirika la habari la Reuters hata hivyo halikuweza kuthibitisha ripoti hiyo ya Getachew ama kuthibisha ni nani hasa aliyeanzisha mapigano kwa kuwa Tigray haina mawasiliano ya simu tangu vikosi vya serikali vilipoondoka zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Soma Zaidi:Ethiopia yailaumu TPLF kwa kutoshirikiana kutafuta amani

Äthiopien | Dr. Legesse Tulu - Kommunikationsminister
Msemaji wa serikali ya Ethiopia Legesse Tulu hakuweza kuthibitisha taarifa za mashambulizi hayo mara moja.Picha: Seyoum Getu/DW

Msemaji wa serikali ya Ethiopia Legesse Tulu, msemaji wa jeshi Kanali Getnet Adane na msemaji wa waziri mkuu Billene Seyoum hata hivyo hawakupatikana mara moja kuzungumzia madai hayo walipoombwa kufanya hivyo. Waziri wa habari wa Eritrea Yeane Gebremeskel pia hakuweza kulizungumzia hilo alipoulizwa kuhusu taarifa hizo.

Serikali ya Ethiopia jana Jumatano ilitoa taarifa ikiwashutumua wanajeshi wa Tigray kwa kuanzisha mashambulizi kadhaa dhidi ya vikosi vya serikali, huku pande hizo mbili zikiendelea kutupiana lawama kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwezi Machi.

Reuters ilizungumza na shuhuda mmoja aliyesema wameshuhudia mizinga mikubwa katika mji wa Shiraro karibu na mpaka wa Eritrea yaliyoanza kurushwa majira ya saa 4.30 alfajiri ya leo. Hata madereva wa misaada ya kiutu wameonekana kuondoka kwenye maeneo hayo ya mpakani.

Äthiopien | Kämpfer der Tigray People's Liberation Front
Baadhi ya wanajeshi wa TPLF wakiwa kwenye harakati zao katika mji wa Hawzen.Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Kiongozi wa wanamgambo katika mji wa Gondar ulioko Amhara ambaye ana mawasiliano na wanajeshi walioko kwenye uwanja wa vita aidha amethibitisha kuweko kwa mapigano makali kutoka upande wao, na kuilenga mitaro ya kijilinda ya wanajeshi wa Tigray katika mji huo wa Shiraro.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken jana jioni aliitolea mwito serikali ya Ethiopia na TPLF kusitisha mara moja operesheni za kijeshi na kushirikiana katika mchakato wa kumaliza mzozo nchini humo.

Eritrea ilipeleka majeshi yake Tigray ili kuwasaidia wanajeshi wa Ethiopia mara tu baada ya kuzuka kwa mapigano Novemba 2020, ingawa mataifa yote mawili yanakana kuhusiana na kupelekwa kwa wanajeshi wa Eritrea nchini Ethiopia.

Soma Zaidi: Ethiopia yatangaza hali ya hatari nchi nzima

Katikati ya mwaka 2021, majeshi ya Ethiopia na Eritrea yaliondoka kwenye maeneo mengi ya Tigray baada ya kuongezeka kwa mapambano na wanajeshi wa Tigray kujificha. Mwezi Januari rais wa Eritrea Isaias Afwerki aliviambia vyombo vya habari kwamba taifa hilo halitasita kuingilia kati iwapo wanajeshi hao wa Tigray watajaribu kuyumbisha tena utulivu nchini Ethiopia.

Soma Zaidi: Amnesty: Wapiganaji wa Tigray walibaka, kupora na kuwapiga wanawake

Mashirika: AFPE/RTRE