1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yailaumu Misri kwa machafuko

10 Oktoba 2016

Serikali ya Ethiopia imeshutumu kuwepo kwa nguvu za nje zinazoongeza fukuto la maandamano katika mkoa wa Oromia, huku ikiituhumu Misri kwa kuyasaidia makundi yaliyopigwa marufuku nchini humo.

https://p.dw.com/p/2R5RR
Äthiopien Protesten der Oromo in Bishoftu
Picha: REUTERS/File Photo/T. Negeri

Hali hiyo ya machafuko inaendelea ikiwa ni siku moja kabla ya ziara ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, inayotarajiwa kufanyika kesho Jumanne. Serikali ya Ethiopia inatuhumiwa na waandamanaji kwa kujimilikisha ardhi na kudharau haki zao za kisiasa. 

Hata hivyo msemaji wa serikali, Getachew Reda, amewaambia waandishi wa habari kwamba, wanachokiona sasa ni kuhusika kwa magenge yenye silaha, ambayo yamesaidiwa kupata silaha hizo, kupata mafunzo na waliowezeshwa kifedha na mataifa kutoka nje. Serikali inaituhumu Misri kuhusika.

Balozi wa Misri nchini Ethiopia tayari amekutana na maafisa wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa gazeti la Daily News la Misri, siku ya Jumapili wizara wa mambo ya nje ilitoa taarifa iliyoeleza kuwa balozi huyo ameihakikishia Ethiopia kwamba Misri haiingilii kwa namna yoyote masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Serikali ya Ethiopia hivi sasa inakabiliwa na changamoto kubwa katika kipindi chake cha miaka 25 ya utawala, kutokana na kusambaa kwa maandamano, kulengwa kwa makampuni ya uwekezaji kutoka nje na kuvurugika kwa hali ya usalama na mauaji ya mamia ya waandamanaji.

Äthiopien Getachew Reda in Addis Abeba
Msemaji wa Serikali ya Ethiopia, Getachew Reda amesema wana uhakika na uhusika wa Misri kwenye machafuko nchini mwake.Picha: DW/Y. Geberegeziabeher

"Kitisho tunachokabiliana nacho hivi sasa, ni mashambulizi ambayo yanawalenga raia pamoja na uwekezaji. Hivi havitaweza kumalizwa kwa kutumia utaratibu wa kawaida wa kisheria tulionao", ameongeza msemaji huyo wa serikali ya Ethiopia, Getachew.

Waandamanaji, wengi wao wakiwa kutoka makabila ya Oromo na Amhara wanasema wamekuwa wakitawaliwa na kundi dogo la kabila la Tigrayan, linaloongoza serikali, ambalo wanalituhumu kumiliki madaraka na kuutawala uchumi wa nchi hiyo. 

Hata hivyo, Getachew amesema adui yao wa asili ambae ni Misri amekuwa akilifunza na kuliwezesha kifedha kundi la waasi la Oromo Liberation Front, OFL, linalochukuliwa na Ethiopia kama kundi la kigaidi na ambalo inasema linahusika na maandamano hayo.

Getachew amesema, "Tunajua kwamba viongozi wa kundi hilo ambao awali walikuwa Asmara, Eritrea, hivi sasa wapo Cairo."

Ethiopia hivi sasa inajenga mradi wa umeme wa kutumia maji kwenye Mto Nile, karibu na bwawa la kuzalisha umeme lililopo nyanda za juu nchini humo. Hatua hii inaamsha hisia za wasiwasi nchini Misri kwamba Ethiopia inataka kuyadhibiti maporomoko ya maji ya mto huo kwa faida yake.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/EAP/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef