Ethiopia yashinikizwa kusimamisha kampeni ya kijeshi Tigray
5 Novemba 2020Vikosi vya wanajeshi wa serikali kuu ya Ethiopia na wale wa jimbo wamepambana kaskazini mwa nchi hiyo jana Jumatano baada ya waziri mkuu Abiy kuwaamrisha wanajeshi wake kujibu shambulio linalodaiwa kufanywa dhidi ya vikosi vya serikali katika jimbo hilo na jeshi la kundi la ukombozi wa watu wa Tigray, TPLF.
TPLF ni kundi lililokuwa na nguvu kubwa ya kisiasa katika muungano uliojumuisha makundi ya makabila yote, uliotawala kwa miongo kadhaa nchini humo, lakini likajiondowa baada ya Abiy ambaye anatokea kabila la Oromo kuingia madarakani miaka miwili iliyopita na kuupangua upya muungano huo na kuufanya chama kimoja.
Nchi za ukanda huo zinahofia kwamba mgogoro huu unaweza kuongezeka na kuwa vita kamili chini ya waziri mkuu Abiy ambaye alitunukiwa tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019 kwa kuufikisha mwisho mgogoro wa miongo kadhaa kati ya nchi yake na jirani yake Eritrea, lakini kwa upande mwingine akiwa anakabiliwa na kuripuka kwa machafuko ya kikabila katika nchi yake.
''Katibu mkuu ameelezea kushtushwa kwake na ripoti za mapigano ya kijeshi katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia na ametowa mwito wa kuchukuliwa mara moja hatua za kumaliza mivutano na kuhakikisha mzozo huo unapatiwa ufumbuzi wa amani. Ametilia mkazo umuhimu wa amani na uthabiti wa Ethiopia kwa ajili ya ukanda wa pembe ya Afrika. na kusisitiza juu ya kujitolea kwa Umoja wa Mataifa na washirika wake katika ukanda huo katika kuinga mkono serikali ya Ethiopia katika juhudi zake zenye lengo la kujenga mustakabali wa amani na usalama kwa watu wake.'' Amesema Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric.
Mivutano na kundi la TPLF imekuwa ikiongezeka tangu mwezi Septemba baada ya jimbo hilo la Tigray kuamua kivyake kufanya uchaguzi wa jimbo na kukaidi uamuzi uliokuwa umepitishwa na serikali kuu wa kusimamisha chaguzi. Serikali kuu ilikataa kuutambua uchaguzi huo wa Tigray ikisema sio halali.
Katika siku za karibuni pande hizo mbili zilishutumiana kila mmoja akidai mwenzake anapanga njama za mgogoro wa kijeshi.
Duru zinasema kwamba harakati zinaendelea chini kwa chini za kuzishawishi pande zote kuingia kwenye mazungumzo ambayo yanatiwa msukumo na Umoja wa Afrika.
Lakini pia inaelezwa kwamba juhudi hizo zinapingwa na maafisa mjini Addis Ababa wanaosema wanabidi wakiondowe kitisho kinachosababishwa na TPLF.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Grace Patricia Kabogo