EU: kuwapeleka waomba hifadhi kwenye mataifa mengine
11 Aprili 2024Fikra ya kuwahamisha waomba hifadhi walioingia ndani ya mataifa wanachama wa kanda ya Umoja wa Ulaya kwa kuwapeleka kwenye nchi nyingine ilionekana kwa mara ya kwanza miezi ya karibuni kupitia mkataba kati ya Italia na Albinia - taifa la Ulaya mashariki lisiyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Vilevile imedhihirika kupitia maguezi ya sheria za uhamiaji na uombaji hifadhi. Mageuzi hayo yanajumuisha kipengele kinachoruhusu waomba hifadhi kupelekwa nchi ya tatu iliyo salama.
Hata hivyo kipengele hicho kinaweka masharti yanayotaka kuwe na alau uhusiano fulani kati ya mwomba hifadhi na nchi anayochaguliwa kupelekwa. Inaweza kuwa kwa msingi wa kitamaduni au asili. Hilo ndiyo linautofautisha mpango wa Umoja wa Ulaya na ule wa Uingereza.
Serikali mjini London yenyewe imeichagua nchi moja tu ya Afrika kuwa kituo cha kuwapeleka waomba hifadhi wote walioingia Uingereza kinyemela. Nayo ni Rwanda. Na msimamo huo tayari umeiletea matatizo serikali ya waziri mkuu Rishi Sunak mbele ya Mahakama ya Haki za Bindamu ya Ulaya kwa sababu hauzingatii msingi wa mwomba hifadhi kuwa na uhusiano na taifa hilo dogo la Afrika ya Kati.
Uingereza, Rwanda zatarajia kuwahamisha wahamiaji wiki chache zijazo
Mkondo huo wa Uingereza hautaweza kufuatwa na Umoja wa Ulaya anaseama Alberto Horst Neidhardt, mtaalamu wa masuala ya uhamiaji anayefanya kazi na kituo cha uchambuzi wa sera cha barani Ulaya. Kulingana na Alberto suala la kuchagua nchi moja kuwa kituo cha kuwapeleka waomba hifadhi wote kutoka mataifa ya Umoja wa Ulaya litakuwa kinyume na sheria za sasa za uhamiaji na wala halitakuwemo kwenye mageuzi yanayopigiwa debe.
Austria na Denmark wanashauku ya kufuatia njia iliyochukuliwa na Uingereza.
Licha ya hayo lakini baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya mfano wa Austria na Denmark wameonesha shauku ya kufuatia njia iliyochukuliwa na Uingereza.
Vilevile kufuatia kuongezeka idadi ya maombi ya watafuta hifadhi barani Ulaya na matarajio ya kufanya vizuri kwa vyama vya mrengo mkali wa kulia katika uchaguzi wa bunge la Ulaya mnamo mwezi Juni vimevifanya vyama vya kihafidhina ndani ya bunge la sasa kutafakari upya msimamo wao.
Na wanasiasa wake wengine inaonesha wanaunga mkono wazo la kutafutwa nchi ya tatu ya kuwapeleka waomba hifadhi wasio na vibali. Kundi la vyama vya kihafidhina ndani ya Bunge la Ulaya kwa kifupi EPP ambalo ndiyo kubwa zaidi ndani ya chombo hicho limeanza kutoa mapendekezo ya kuwahamisha haraka waomba hifadhi kwenye nchi ya tatu.
UN yaitaka Uingereza kuachana na mpango wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda
EPP ambalo ni kundi linalomjumuisha rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen wameliweka pendekezo hilo ndani ya ilani yake ya uchaguzi wa mwezi Juni. Jens Spahn, mwanachama wa chama cha kifadhina Christian Democratic Union cha nchini Ujerumani kilicho sehemu ya kundi la EPP amesema idadi ya wahamiaji wanaojaribu kuingia Ulaya itapungua ikiwa watafahamu kuwa ndani ya saa 48 baada ya kuwasili kwao wataondolewa na kupelekwa kwenye nchi nyingine isiyo mwanachama wa kanda hiyo.
Yeye amekwenda mbali zaidi na hata kupendekeza mataifa kama Rwanda, Georgia au Moldova kuwa yanafaa kwa mpango kama huo.
Serikali ya Meloni yaunga mkono kuanzisha vituo vya kuwapokea wahamiaji
Serikali ya mrengo wa kulia nchini Italia ya waziri mkuu Giorgia Meloni imeingia mkataba na Albania kuanzisha vituo vya kuwapokea wahamiaji wanaoingia kwa njia ya bahari. Mkataba huo uliosainiwa mwezi Novemba kwenye mji mkuu wa Albania, Tirana unasema wahamiaji watapelekwa kwenye vituo vya kuwazuia kwa muda nchini Albania. Vituo hivyo vitaendeshwa na kulipiwa na Italia ambayo itafanya kazi ya kuchambua maombi ya wahamiaji wote kwa mujibu wa sheria za Italia.
Rais wa Halmashuari Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen aliutaja mkataba huo kuwa wa mfano. Kwa Jean-Louis De Brouwer, afisa wa zamani wa ngazi ya juu kwenye kamisheni ya uhamiaji barani Ulaya anasema mkataba kati ya Italia na Albania unaweza kusambaa kwa sababu kuna kiambata cha kisiasa ndani yake. Hasa kwa mataifa yaliyosaka uanchama ndani ya Umoja wa Ulaya. Kwa maoni yake hiyo ni nafasi kwa nchi hizo kuonesha kwamba ziko tayari kujitoa kwa mshikamano kushughulikia wimbi la uhamiaji.
Brouwer anasema nchi hasa za kanda ya Balkani ambazo zinawania kuwa wanachama wa kanda ya Ulaya kwa miaka mingi hazitosita kuridhia mkataba wa aina hiyo. Na katika wakati makundi ya hisani yanapinga sera za sasa za Umoja wa Ulaya zinazoweka vigingi kwa wahamiaji, mataifa ya kanda hiyo yataona ndiyo muda mwafaka wa kuhamishia mizigo huo kwa nchi nyingine za Ulaya zisizo wanachama kwa sababu haziwezi kuandamwa na sheria za kanda ya Ulaya.
dpa