EU kutoa msaada kukabiliana na athari za mafuriko Afrika
26 Septemba 2024Umoja wa Ulaya umetoa euro milioni 5.4 za msaada kwa ajili ya nchi sita za Afrika Magharibi na Afrika ya Kati zilizoathiriwa na mafuriko yaliyosababisha vifo.
Taarifa hiyo imetolewa jana Jumatano na ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Chad ukisema msaada huo unanuiwa kuwasaidia watu walioathiriwa vibaya kabisa kufuatia mafuriko nchini Chad, Niger, Nigeria, Cameroon, Mali na Burkina Faso.
Umoja wa Ulaya unaipa Niger euro milioni 1.35, Nigeria euro milioni 1.1, na Chad na Mali euro milioni moja kila nchi. Cameroon imetengewa euro 650,000 na Burkina Faso euro 350,000.
Tangu msimu wa mvua ulipoanza, mvua kubwa zimekuwa zikinyesha katika baadhi ya maeneo. Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na uhamiaji, IOM, kufikia sasa mvua hizo zimewaua watu zaidi ya 1,500, kuwaathiri watu milioni nne na kuwalazimu wengine milioni 1.2 kuyahama makazi yao katika nchi hizo sita, pamoja na Guinea.