1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waitaka Uingereza kuzingatia sheria

Isaac Gamba
30 Machi 2017

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekumbusha kuwa Uingereza italazimika kuzingatia taratibu zote za kisheria hadi itakapokamilisha kipindi cha miaka miwili cha mchakato wa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/2aJAI
Brüssel Donald Tusk zu Brexit
Picha: Reuters/Y. Herman

Katika taarifa yake rasmi baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May kuanzisha rasmi mchakato wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel alisema  Ujerumani inafurahi kwa sabababu kusubiri kumefika mwisho. Alisema nchi 27 zilizosalia kwenye umoja huo zinaelewa nini wanataka kwa sasa  kuhusiana na mustakabali wa Umoja wa Ulaya na kuongeza kuwa katika hilo wana msimamo ulio wazi na kuwa wataipa  Halmashauri ya Ulaya mamlaka zaidi kusimamia  misingi ambayo nchi hizo zingependelea iheshimiwe katika kipindi cha miaka miwili cha mazungumzo hayo ya Brexit.

Hata hivyo waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani alisema pande zote mbili zinahitajiana  na kuwa Umoja wa Ulaya utafanya kila linalowezekana kuendeleza uhusiano mzuri na Uingereza katika siku za usoni.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Brussels mara baada ya kupokea waraka uliowasilishwa na balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Ulaya Tim Farrow kuashiria  kuanzisha rasmi mazungumzo ya mchakato huo, rais wa baraza la Ulaya Donald Tusk alisema haikuwa siku nzuri kwa pande zote mbili iwe kwa Uingereza au kwa Umoja wa Ulaya kwani raia wengi wa Ulaya ikiwa ni pamoja na nusu ya wapiga kura nchini Uingereza wangependelea isalie kwenye Umoja wa Ulaya.

Kwa upande wake Rais wa Bunge la Ulaya Antonio Tajani alisema haikuwa siku nzuri kwa Ulaya  kwani ni mara ya kwanza nchi mwanachama imeamua kutengana nao ingawa Umoja wa Ulaya unaheshimu haki ya kidemokrasia ambayo Waingereza walio wengi wameitumia na kuamua  kujiengua kwenye umoja huo.

EU-Gipfel auf Malta | Angela Merkel & Theresa May
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Kansela Merkel kuhakikisha mazungumzo ya Brexit yanakuwa na mafanikio

Katika hotuba yake mjini Berlin Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema pande zote mbili zitapaswa kwanza kukubaliana juu ya taratibu jinsi gani Uingereza itajiengua kwenye  Umoja wa Ulaya kabla ya  kuendelea na hatua nyingine. Aidha Kansela Merkel alisisitiza kuwa atahakikisha mazungumzo ya mchakato  wa Brexit yanakuwa na mafanikio kwa pande zote mbili.

Aliongeza kuwa sio siri kwamba Umoja wa Ulaya ukiongozwa na Ujerumani hautakubali kuruhusu Uingereza kuendelea kufaidika na soko la pamoja la Ulaya labda kama  Uingereza itawahakikishia kuwa kutakuwa na uhuru wa watu kusafiri, bidhaa kuingia na kutoka pamoja na huduma.

Waziri wa Uingereza anayehusika na masuala ya Brexit David Davis alisema Uingereza hailengi kuitisha ulaya wakati iliposema ushirikiano katika kupambana na ugaidi utadhoofika iwapo itajiondoa kwenye Umoja wa Ulaya pasipo makubaliano yanayokubalika na kuongeza kuwa nchi zote zitaathirika iwapo hawatafikia maubaliano yanayoridhisha. Amesema wanalenga katika kuhakikisha kuwa wanaafikiana katika masuala yanayohusiana na ulinzi na nyanja nyingine za mahusiano.

Mwandishi: Isaac Gamba/dw

Mhariri: Iddi Ssessanga