EU yasaka msimamo wa pamoja juu ya Syria
16 Aprili 2018Baada ya Syria kushambuliwa na kikosi kilichoongozwa na Marekani,Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya wanajiandaa kujaribu kuunga mshikamano katika mazungumzo ya pamoja yanayofanyika mjini Luxembourg leo,licha ya kuwepo mgawanyiko kuhusiana na mashambulizi hayo.Kadhalika Umoja huo wa Ulaya unataka kujaribu kuangalkia jinsi ya kushughulikia mgogoro wa kidiplomasia ulioibuka na Urusi kufuatia suala la Syria.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanataka kufikia mtazamo wa pamoja na hatimaye kuwa na mshikamano kufuatia mgawanyiko uliojitokeza juu ya mashambulizi ya Syria. Licha ya kwamba Kansela Angela Merkel ambaye ni kiongozi mwenye nguvu barani Ulaya ametangaza kwamba mashambulizi yaliyofanywa na Marekani, Uingereza na Ufaransa ni hatua iliyohitajika na ya sawasawa, wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya wanapinga kuchukuliwa hatua ya aina yoyote ambayo inaweza kusababisha mgogoro huo kuongezeka.
Wakati wanachama 28 wa Umoja huo wakikubaliana kwamba tukio la kutumika silaha za sumu Syria halikubaliki lakini zimeshindwa kwa pamoja kuridhia kuunga mkono mashambulizi yaliyofanywa. Kwa maana hiyo nchi za Umoja wa Ulaya zimegawika, upande mmoja zikijikuta Ufaransa,na Uingereza na upande mwingine zikiweko zile zisizotaka kuegemea upande wowote na katikati wakiwemo wanachama mbali mbali wa jumuiya ya kujihami ya NATO wenye mtizamo tafauti juu ya mashambulizi dhidi ya Syria. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas, anasema Umoja wa Ulaya unatakiwa kushikamana wakati huu.
Waziri Maas amesisitiza kwamba mgogoro wa Syria hauwezi kutatuliwa bila ya Urusi akisema kwamba anataka kuona mchango kamili wa nchi hiyo. Mkutano wa leo utajadili jinsi ya kuishinikiza Urusi kujaribu kuumaliza mgogoro wa Syria, ingawa hadi sasa nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya zimeshindwa kuzungumzia hatua ya kushambuliwa Syria kwa sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu msimamo utakaotoka Urusi ambayo miongoni mwa mengine ni nchi muhimu inayosambaza gesi barani Ulaya.
Kwa upande mwingine waziri mkuu wa Uingereza Theresa May atakabiliwa na hatua za kukosolewa hii leo kwa kitendo cha kulikiuka bunge kuingia katika mashambulizi dhidi ya Syria. May anatarajiwa kutoa tamko bungeni juu ya uamuzi wake wa kujiunga na Marekani na Ufaransa siku ya Jumamsoi kuishambulia Syria.
Nchi za Kiarabu nazo katika mkutano wake wa kilele jumapili zimetaka kufanyike uchunguzi wa Kimataifa juu kile ilichokiita uhalifu wa kutumia silaha za sumu nchini Syria pamoja na kulaani hatua ya Iran ya kuingilia kati masuala ya nchi nyingine. Hata hivyo jumuiya hiyo ya nchi za kiarabu imejizuia kuzungumza chochote juu ya kuunga mkono mashambulio ya nchi za Magharibi Syria na badala yake zimesisitiza haja ya suluhisho la kisiasa katika mgogoro huo. Kwa upande mwingine mjumbe wa Marekani katika shirika la kudhibiti silaha za sumu OPCW balozi Kenneth Ward amedai kwamba Urusi huenda imevuruga eneo linalodaiwa kutokea shambulio la silaha za sumu huko Douma.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Josephat Charo