F1: Ricciardo aibuka mshindi nchini China
16 Aprili 2018Muasutralia huyo alichukua usukani katika mzunguko wa 45 baada ya kumpiku dereva wa Mercedes Valtteri Bottas. Bottas alimaliza katika nafasi ya pili huku Kimi Raikkonen wa Ferrari akipanda jukwaani katika nafasi ya tatu.
Mjerumani Sebastian Vettel ambaye ameshinda mikondo miwili ya kwanza msimu huu, alimaliza katika nafasi ya nane baada ya kuanza mashindano hayo akiwa katika nafasi ya kwanza. Pia aligongana na dereva wa Red Bull Max Verstappen na hivyo akapoteza nafasi kadhaa. Vettel bado anaongoza msimamo wa ubingwa wa dunia msimu huu akiwa na pointi 54, baada ya mikondo mitatu.
Lewis Hamilton, bingwa mara nne wa dunia na ambaye anatetea taji hilo, alimaliza katika nafasi ya nne na mpaka sasa ana pointi 43. Bottas ana pointi 40 katika nafasi ya tatu kabla ya mkondo ujao wa Azerbaijan.
Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Josephat Charo