1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani kutawazwa Bingwa Uhispania au Uholanzi ?

Mohamed Dahman11 Julai 2010
https://p.dw.com/p/OGNp
Paul der Tintenfisch Oktopus Orakel Spanien Deutschland Halbfinale 2010
Pweza Paul atabiri ushindi ni wa Uhispania.Picha: AP

Mashabiki wa kandanda duniani wanasema kwamba mechi zinazotia fora katika michuano ya kuwania ubingwa wa soka Kombe la Dunia mara nyingi zinakuwa zile za nusu fainali.Lakini kufuatia uwezo wa kuonyeshana kabubmbu la kiwango tafauti timu hizo mbili Uholanzi na Uhispania zinatambuliwa kwa kusakata gozi kiufundi, kimbinu na kuamsha msisimko.Hivyo fainali ya leo inatarajiwa kuwa ya msisimko wa aina yake.

Ni fainali ambayo itaandika upya historia ya kombe la Dunia kwani timu hizo zote mbili hazikuwa kuwa bingwa wa dunia na yeyote atakayelinyakua kombe hilo itakuwa ni mara ya kwanza na mara ya kwanza kwa timu kutoka Ulaya kulinyakuwa kombe hilo katika bara jengine. Uholanzi lakini iliwahi kufika fainali mara mbili, 1974 ilichuana na Ujerumani bila mafanikio na hali hiyo ikajirudia katika fainali ya 1978 ilipomenyana na Argentina.Kama ule usemi halali mara tatu unafanya kazi leo itakuwa zamu ya Waholanzi.

Ikumbukwe pia kwamba hii itakuwa fainali ya kwanza ya Kombe la Dunia ambayo haihusishi timu kama Brazil,Argentina,Italia au Ujerumani ambayo hapo jana imemalizia nafasi ya tatu katika michuano hiyo kufuatia ushindi wa mpambano mkali kati yake na Uruguay katika uwanja wa Port Elizabeth.Goli lilowekwa wavuni kwa kichwa na Sami Khedira zikiwa zimebakia dakika nane tu kabla ya kipenga cha mwisho limeipa ushindi Ujerumani wa mabao 3-2 katika mchuano huo wa kuvuta nikuvute dhidi ya Uruguay.Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Ujerumani kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Dunia.

Somo ambalo pengine wachezaji na mashabiki wa kabumbu watakuwa wamejifunza katika michuano ya mwaka huu ya Kombe la Dunia ni kutamba kwa timu zinazocheza kama kitu kimoja kwa wachezaji kutegemeana kama ilivyothibitishwa na timu za Uhispania na Uholanzi na kuvuna matunda ya kuingia fainali kule mtindo wa kutegemea zaidi wachezaji nyota waliowekewa matumaini makubwa katika michuano hii kama akina Cristiano Ronaldo na Wayne Rooney.

Mabingwa wa Ulaya Uhispania walianza michuano hiyo kwa mwendo wa kobe na kuja kucharukwa kwa kuichachafya timu ya vijana wadodo ya Ujerumani katika mchuano wa nusu fainali imekuwa ikipigiwa debe kunyakuwa ubingwa huu wa soka wa dunia juu ya kwamba imekuwa ikishindwa kutumia vizuri umahiri wa wachezaji wake wa viungo katika kuzifuma nyavu.

Timu hiyo imekuja kushabikiwa na wengi kuanzia watoto wanaosakata kabumbu katika kitongoji cha Soweto hadi vyombo vya habari vya kimataifa vilivyoandika kwamba wachezaji wake sio tu wametulia bali wameonyesha pia jinsi ya kabumbu linavyopaswa kuchezwa

Hata pweza Paul wa Ujerumani aliegeuzwa mpiga ramli na kutabiri kwa usahihi matokeo yote ya mechi za Ujerumani ameitabiria ushindi timu hiyo na isitoshe hata kasuku wa India alieko Malaysia ambaye pia hutumika kupiga ramli ameungana na Paul kuitabiria ushindi Uhispania.

Hata hivyo haitakuwa rahisi hivyo kuibwaga Uholanzi ambapo wachezaji wake akina Dirk Kuyt,Wesley Sneider na Arjen Robben wanatazamiwa kukabiliana ipasavyo na wachezaji mahiri wa viungo wa Uhispania wakiongozwa na Xavi na Andreas Iniesta.

Inafaa izingatiwe kwamba licha ya Wadachi kuwavunja moyo mashabikli wao kwa kucheza mchezo wa kijihami zaidi kulinganisha na timu za zamani za nchi hiyo imeshinda mechi zote za Kombe la Dunia ikiwa ni pamoja na zile za kuwania tiketi ya kushiriki michuano hiyo na ikishinda fainali hii itakuwa timu ya pili kupata ushindi wa aina hiyo ikitanguliwa na Brazil hapo mwaka 1970.

Uhispania inasifiwa kwa uwezo wa kudhibiti mpira na pasi zao za uhakika juu ya kwamba hupata kigugumizi cha mguu wanapoukabili wavu.Imevuna magoli saba tu katika mechi sita.

Uholanzi inayohesabiwa kuwa ni timu nzuri ambayo haikuwahi kamwe kulinyakuwa Kombe la Dunia pia inakosa umaliziaji mzuri wa kufunga magoli wakati muafaka.Angalau timu hiyo ina magoli 12 kibindoni

Fainali ya leo inatazamiwa kuangaliwa na watazamaji milioni 500 duniani kote na ni nafasi ya mwisho kwa kuonyesha tukio ambalo kwa kiasi kikubwa limezima hofu ya waliokuwa na mashaka juu ya uwezo wa Afrika Kusini kuandaa michuano ya soka Kombe la Dunia kwa mafanikio.

Afrika Kusini ilikuwa ikikabiliwa na ripoti mbaya za vyombo vya habari vya kigeni kwamba michuano itageuka kuwa janga kwa kuchafuliwa na vitendo vya uhalifu, fujo na viwanja vya soka kutomalizika kwa wakati uliopangwa.

Wakati mpira ukidunda vuvuzela zinatarajiwa kuendelea kuhanikiza leo usiku katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg hadi kipenga cha mwisho kitapoamuwa nani anastahiki kutawazwa bingwa mpya wa soka wa dunia na kuondoka la taji la Kombe la Dunia.

Ni nani huyo Uhispania au Uholanzi?

Mwandishi:Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman