1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fatou Bensouda aanza kazi ICC

Admin.WagnerD15 Juni 2012

Mwendesha mashtaka Mkuu mpya wa mahakama ya Kimataifa ya makosa ya jinai ICC, Fatou Bensouda anaanza kazi rasmi tarehe 15.06.2012. Lakini ni changamoto zipi zilizopo mbele ya mwanamama huyo kutoka Gambia?

https://p.dw.com/p/15El0
Fatou Bensouda.
Fatou Bensouda.Picha: CC BY-SA 3.0

"Mara nyingi unafanya kazi katika hali ya muendelezo wa migogoro, na hali ya usalama wakati mwingine inafanya utekelezaji wa majukumu usiwezekane bila kuhatarisha usalama wa mashahidi," Bensouda aliliambia shirika la habari la Ujerumani, dpa katika mahojiano maalumu, na kuongeza kuwa katika mazingira kama hayo, kazi inakuwa na changamoto kubwa.

Fatou alikuwa naibu mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC tangu mwaka 2004 na pia aliwahi kuwa Mwanasheria mkuu na mshauri wa rais katika nchi yake ya Gambia. Fatou alisema changamoto kubwa inayomkabili ni kukosa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya mataifa yaliyosaini mkataba wa uanzishwaji wa mahakama hiyo.

Mahakama ya ICC ikisikiliza kesi.
Mahakama ya ICC ikisikiliza kesi.Picha: AP

Hatuna Jeshi wala Polisi
Alisema Mahakama ya ICC haina jeshi na wala haina polisi lakini polisi na majeshi ya mataifa 120 wanachama ndiyo polisi wa ICC na hivyo wana wajibu wa kusaidiana na mahakama hiyo katika kuwakamata watu kama kiongozi wa kundi la waasi la LRA Joseph Kony, rais wa Sudan Omar Hassan el Bashir, lakini akasema kuwa inasikitisha kuona watu hao bado hawajafikishwa mbele ya sheria.

Alivyoulizwa endapo mahakama ya ICC inavuruga utulivu wa kisiasa katika nchi kutokana na uchunguzi wa makosa ya jinai, Bensouda alisema kinyume chake, uchunguzi huo kwa mfano nchini Uganda, umechangia kwa kiwngo kikubwa kurejesha amani kaskazini mwa nchi hiyo licha ya ukweli kwamba hawajaweza kumkata Joseph Kony.

Alisema pia katika nchi ya Cote d' Vior, mahakama ya ICC pia imetoa mchango mkubwa. Tangu mwanzo tulisema tutafanya uchunguzi na tunangali pande zote zilizokuwa katika mgogoro huu. Kesi ya Laurent Gbagbo ndiyo ya kwanza....bila shaka kutakuwa na wengine, alisema.

Shutuma za kutumiwa na mataifa makubwa
Bensouda alisema changamoto nyingine inayoikabili mahakama hiyo ni juu ya shtuma zinazotolewa kwake kuwa inatumiwa na baadhi ya mataifa kuyaadhibu mataifa mengine huku pia ikilaumiwa kwa kesi ambazo zimeshindwa kufikishwa mbele yake, akitolea mfano wa Syria, ambayo hata hivyo alisema haikuridhia Mkataba wa Rome uliyoanzisha mahakama hiyo na hivyo si mwanachama wa ICC.

Alisema mahakama hiyo inaweza tu kuingilia kati nchini Syria kama Umoja wa mataifa utaitaka ifanye hivyo. hata hivyo, alisema kuanza mchakato wa kufungua mashtaka unaweza kuchukua muda mrefu kwa vile unahitaji uchunguzi wa hali juu kuweza kuja na ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashataka wahusika, tofauti na inavyoonekana hivi sasa.

Mwendesha Mashtaka Mkuu anliyemaliza muda wake, Luis Moreno-Ocampo.
Mwendesha Mashtaka Mkuu anliyemaliza muda wake, Luis Moreno-Ocampo.Picha: AP

Mwendo ni ule ule!
Bensouda alisema licha ya tuhuma kwamba mahakama ya ICC inawalenga waafrika pekee, kuwepo kwake katika nafasi ya mwendesha mashataka mkuu hakutaleta tofauti yoyote na kwamba ataendelea kuonyesha kuwa ICC inafanya kazi kwa ajili ya, na pamoja na waathirika wa Afrika, kwa sababu waathirika wote katika migogoro inayofikishwa mbele ya mahakama hiyo ni waafrika.

Bensouda anamrithi Luis Moreno Ocampo aliejipatia umaarufu kutokana na kuendesha kesi kadhaa zenye msisimko mkubwa ikiwa ni pamoja na rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor, aliyehukumiwa hivi karibuni kwenda jela kwa miaka 50, na kudiriki kumuombea kibali cha kukamatwa, rais wa Sudan Omar el Bashir, ambaye hata hivyo Umoja wa Afrika unapinga kukamatwa kwake.

Ocampo alikuwa akishtumiwa kwa kutumia ubabe katika kipindi cha uongozi wake na inadaiwa wafanyakazi wengi wa juu wa idara yake walilaazimika kuacha kazi. Lakini Besnouda, ambaye hakukanusha tuhuma hizo dhidi ya bosi wake wa zamani alisema jambo la muhimu sasa ni kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\DPAE
Mhariri: Saum Yusuf.