Fatou Bensouda apokonywa kibali cha kuingia Marekani
5 Aprili 2019Ofisi ya mwendesha mashitaka huyo wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhaliifu, ICC, imesema kile inachoweza kuthibitisha kwa sasa ni kwamba kibali cha kuingia nchini Marekani cha Fatou Bensouda kimefutwa, huku ikisema katika taarifa yake kwamba mwendesha mashitaka huyo ataendelea na majukumu yake bila uwoga au fadhila kwa mtu yeyote.
Mwezi uliopita Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Mike Pompeo alisema Marekani ingelifuta au kumyima kibali afisa yeyote wa ICC anayetaka kuanzisha uchunguzi wa madai kama hayo dhidi ya wanajeshi wa Marekani au washirika wake.
Lakini Ofisi ya Fatou Bensouda imesema uamuzi wa Marekani haukutarajiwa kuathiri safari zake ndani ya Marekani kutekeleza majukumu yake katika Umoja wa Mataifa.
Mahakama ya ICC sio chombo cha Umoja wa Mataifa, lakini Bensouda huenda mara kwa mara kutoa ripoti kwenye Baraza la Usalama huo juu ya kesi zilizowasilishwa kwake na Umoja huo.
Wataalamu wa kutetea haki za binaadamu wakosoa uamuzi wa Marekani
Ofisi ya Bensouda imesema chini ya Mkataba wa Roma unaounda mahakama ya ICC ambapo Marekani ilikataa kujiunga nao tangu mwaka 2002, bado Bensouda ana mamlaka huru yasioegemea upande wowote. Urusi na China, mataifa yalio na nguvu duniani pia sio wanachama wa ICC.
Hata hivyo, wataalamu wa kutetea haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa wameitaja hatua hiyo ya Marekani kama kuingilia kazi ya mahakama ya hiyo ya kimataifa iliyo na jukumu la kuchunguza uhalifu wa kivita. Hatua hiyo ya Marekani pia imekosolewa ndani ya Umoja wa Ulaya. Marekani kwa upande wake haijatoa tamko lolote juu ya suala hili.
Fatou Bensouda amekuwa akichunguza madai ya uhalifu wa kivita katika pande zote kwenye mgogoro wa Afghanistan kuanzia mwezi Novemba mwaka 2017, ikiwemo uwezekano wa jumuku la watumishi wa Marekani kuhusiana na kufungwa kwa washukiwa. Majaji wa mahakama hiyo bado wanaangalia ushahidi na bado hawajatoa uamuzi wao wa kuanzisha rasmi uchunguzi juu ya uhalifu wa kivita nchini Afghanistan.
Mahakama ya ICC ina wanachama 122 na inachukua hatua tu wakati mataifa yaliyo wanachama wake yatapatikana au kuonekana kushindwa kuchunguza uhalifu wa kivita, mauaji ya kimbari au makosa makubwa ya mateso.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef