Rais Biden awaamuru FBI kuweka hadharani uchunguzi Sept. 11
12 Septemba 2021Jamaa wa wahanga wa mashambulizi hayo walikuwa wamemtaka Rais Biden kutohudhuria mikusanyiko ya kumbukumbu ya miaka 20 iliyofanyika siku ya Jumamosi (Septemba 11), endapo hakuziweka hadharani nyaraka ambazo wanaamini zingelionesha kwamba mamlaka nchini Saudi Arabia zilisaidia hujuma hiyo kutendeka.
Sehemu ya waraka huo wenye kurasa 16 iliyotolewa siku ya Jumapili (Septemba 12) inabanisha mawasiliano baina ya watekaji nyara na washirika wao wa Kisaudi, lakini ndani yake hamuna ushahidi wowote kwamba serikali mjini Riadh ilihusika na mashambulizi hayo yaliyouwa takribani watu 3,000.
Kwa muda mrefu, Saudi Arabia imekuwa ikisema kwamba haihusiki kwa namna yoyote na mashambulizi hayo.
Ubalozi wa nchi hiyo jijini Washington haukujibu ombi la kuzungumzia uwekwaji huo hadharani wa nyaraka za siri za uchunguzi wa kijasusi, lakini kwenye taarifa yake ya tarehe 8 Septemba, ubalozi huo ulisema Saudi Arabia daima imepigania uwazi kwenye matukio yanayohusiana na tarehe 11 Septemba 2001 na inafurahia hatua ya kutolewa kwa nyaraka hizo.
"Kama uchunguzi wa zamani ulivyobainisha, ukiwemo wa Kamisheni ya 9/11 na kutolewa kwa kile kiitwacho 'Kurasa 28', hakujakuwapo ushahidi wowote unaoonesha kwamba serikali ya Saudia ama maafisa wake walikuwa wanajuwa kuhusu mashambulizi haya ya kigaidi au kwamba walishiriki kwa namna yoyote ile," ulisema ubalozi huo kwenye taarifa yake.
Kutokuhusika kwa Saudi Arabia
Licha ya kwamba watekaji nyara 15 kati ya 19 walikuwa wanatoka Saudi Arabia, kamisheni hiyo iliyoundwa na serikali ya Marekani haikupata ushahidi kwamba Saudi Arabia ililifadhili moja kwa moja kundi la kigaidi la Al-Qaida, ambalo lilikuwa likipewa hifadhi na Taliban nchini Afghanistan kwa wakati huo.
Hata hivyo, ripoti ya kamisheni hiyo haikusema ikiwa watu binafsi na waliokuwa maafisa wa serikali ya Saudi Arabia walihusika ama la.
Familia za takribani watu 2,500 ya wale waliouawa na zaidi ya watu 20,000 waliojeruhiwa na wawakilishi wa kampuni za kibiashara na za bima wameifungulia mashitaka Saudi Arabia wakitaka fidia ya mabilioni ya dola.
Licha ya nyaraka za FBI kuivua serikali ya Saudi Arabia na lawama za mashambulizi hayo, Terry Strada, ambaye mumewe Tom aliuawa siku ya Septemba 11 na anayewakilisha jumuiya ya familia za wahanga wa mashambulizi hayo, alisema nyaraka zilizowekwa hadharani siku ya Jumamosi na FBI zinaondowa mashaka yoyote juu ya ushiriki wa Saudia.
"Sasa siri za Wasaudia zipo hadharani na umefika wakati kwa Ufalme huo kubeba dhamana ya maafisa wake kwa kuwauwa maelfu ya watu katika ardhi ya Marekani," ilisema taarifa iliyosomwa na Strada.