FC Kolon iko njia panda hadi sasa ina pointi mbili
23 Oktoba 2017Hoffenheim walilazimika kukubali sare ya bao 1-1 dhidi ya Wolfsburg wakati FC Kolon na Werder Bremen zimeendelea kubakia bila ushindi katika msimu huu wa Bundesliga baada ya kutoka sare jana bila kufungana. FC Kolon ambayo inashika mkia katika msimamo wa ligi imepata pointi yake ya pili msimu huu baada ya michezo tisa. Kocha wa FC Kolon Peter Stoger amesema ilikuwa bahati mbaya kwamba kikosi chake hakikuzawadiwa pointi tatu muhimu.
"Yalikuwa mapambano makali. Mipango katika mchezo huu haikuwa kama tulivyoipanga , ama kama vile timu inapokuwa katika hali hii inavyotakiwa kucheza, na kutokana na hali ilivyo haikuwa mbaya sana.
Nafikiri , timu zote mbili zilichukua hatua zote zinazostahili. Kulikuwa na nafasi nyingi za kufunga mabao , na kushinda mchezo huo. Kwa matokeo haya, hakuna kati yetu anayeweza kwa usahihi kuanzisha kitu. Ndio sababu tathmini yangu kuhusu mchezo huu ni kwamba nilichokitaka , vijana wangu wamekifanya. Kumekuwapo na hamasa kubwa katika mchezo huu bila shaka."
Kocha wa Bremen Alexander Nouri amesema kikosi chake kilipoteza udhibiti wa mipira mara kwa mara na kwamba hiyo ni sehemu mijawapo ambayo wachezaji wake wanapaswa kufanyia kazi.
Hoffenheim iko katika njia salama
Licha ya sare ya bao 1-1 Hoffenheim ilipanda na kujiweka katika nafasi ya nne ya msimamo wa ligi , huku Bayern Munich baada ya ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Hamburg SV ambayo ilicheza kwa kipindi kirefu cha mchezo huo ikiwa na wachezaji 10 uwanjani imefikisha pointi 20 sawa na Borussia Dortmund ambayo katika muda wa wiki mbili zilizopita imekuwa ikisuasua na kuonesha udhaifu katika safu yake ya ulinzi.
Dortmund ilitoka sare ya mabao 2-2 na Eintracht Frankfurt baada ya kuongoza kwa mabao 2-0. Huyu hapa mshambuliaji wa pembeni wa Borussia Dortmund Maxmillian Philipp.
"Tumefadhaika mno , na hii inaweza kuonekana katika nyuso zetu. Tulifanya kazi kubwa. Tulijua kuwa Frankfurt ni timu nzuri, ambayo inaonesha uwezo mkubwa. Na leo wamefanya hivyo. Sijui , iwapo tulidhani kila kitu kimemalizika. Kwa kuongoza kwa mabao 2-0 hili halikupaswa kutokea, katika muda wa dakika tano tunafungwa mabao 2, inaumiza."
RB Leipzig ni ya tatu baada ya kuishinda Stuttgart kwa bao 1-0.
Leverkusen yacharuka
Bayer Leverkusen iliirarua Borussia Moenchengladbach kwa mabao 5-1 na kujiimarisha zaidi katika msimamo wa ligi ambapo hivi sasa iko nafasi ya tisa ikiwa na pointi 12 nyuma ya Gladbach ambayo ina pointi 14 ikiwa katika nafasi ya 8.
Michuano ya kombe la shirikisho nchini Ujerumani DFB Pokal duru ya pili inarejea uwanjani kesho Jumanne na Jumatano , ambapo michuano muhimu ni inatarajiwa kuwa siku ya Jumatano, ambapo RB Leipzig inaikaribisha Bayern Munich na Bremen ikipambana na Hoffenheim.
Pambano la RB Peipzig na Bayern Munich linavuta hisia za mashabiki wa soka hapa Ujerumani baada ya Bayern kumrejesha kocha wake wa zamani Jupp Heynckes kukinoa kikosi hicho ambacho kilikuwa kikinolewa na kocha Mtaliani Carlo Anchelotti.
Bayern Munich haijapata changamoto kubwa kutoka kwa vijana hao wa Leipzig tangu waingia katika ligi daraja la kwanza msimu uliopita. Katika ligi Leipzig haija fua dafu mbele ya miamba hao kutoka Munich, ambapo katika mchezo wa kwanza walibugia mabao 3-1 na mchezo wa pili Bayern Munich ilishinda kwa mabao 5-4.
Hivyo macho yote yatakodolewa siku ya Jumatano katika mchezo huo ambapo vijana wa Leipzig wakiwa nyumbani wanatarajia makubwa.
Ikiwa wataitoa Bayern katika DFB Pokal itakuwa ni mara ya kwanza Bayern kuaga mashindano haya katika duru ya pili.
Kesho Jumanne Borussia Dortmund inapambana na Magdeburg timu ya daraja la tatu , wakati Schalke 04 inakwaana na Wehen Wiesbaden pia ya daraja la tatu. Leverkusen inapambana na Union Berlin na Mainz inakwaana na Kiel iliyoko daraja la pili.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul rahman