1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mageuzi yahitajika

11 Januari 2016

Kisa cha kufedhehesha kilichotokea mkesha wa mwaka mpya mjini Cologne na athari zake pamoja pia na mzozo wa Poland ndizo mada zilizohodhi magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1HbDk
Zeitungscover - Focus
Toleo la Jarida la Focus kuhusu mkasa wa mkesha wa mwaka mpya-Wanawake watuma mashitakaPicha: Focus

Tuanzie lakini na kisa kilichotokea mkesha wa mwaka mpya katika jiji la Cologne. Gazeti la Ludwigsburger Kreiszeitung linaandika: "Utafiti wa maoni ya umma umedhihirisha asilimia 48 ya Wajerumani wanataka hivi sasa kiwekwe kikomo cha idadi ya wakimbizi wanaoingia kwa mwaka humu nchini. Hali hiyo haimaanishi kwamba nusu ya wakaazi wa Ujerumani wanaunga mkono siasa kali za mrengo wa kulia. Ila tu wanataka wanasiasa waweke kando nadharia zao za mkwamo katika suala la wakimbizi."

Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linahisi:"Si suala tena hilo kwamba maafisa wa serikali watachukua hatua zinazostahiki dhidi ya wakimbizi wanaohusika na uhalifu, ikiwa ni pamoja na kuwarejesha kule kule walikotokea. Ili kulitekeleza hilo hakuna sheria mpya zinazohitajika,ila tu kupata maelezo kuhusu wale waliofanya visa vya uhalifu. Stuttgarter Nachrichten linazungumzia pia kuhusu upungufu wa polisi unaoshuhudiwa tangu mwaka 1998. Wito wa wanasiasa wa ngazi ya juu kutoka vyama vya CDU na FDP katika jimbo la North Rhine Westphalia kutaka hadi polisi 1500 waajiriwe unatajwa na gazeti hilo la mjini Stuttgart kuwa ni sawa na kuungama kwamba vyama vyao havikufanya vya kutosha miaka iliyopita katika suala la usalama.

Mabaadiliko yanawezekana

Nalo gazeti la "Nürnberger Zeitung linaamini kansela anaweza kubadilisha msimamo wake. Ushahidi ulioonekana baada ya janga la Fukushima. Wakati ule aliamua kuanzisha mageuzi katika sera ya nishati na kujipatia uungaji mkono mkubwa miongoni mwa wananchi. Na hata katika suala la kukaribishwa wakimbizi marekebisho yanawezekana. Kwa wakati wote ule ambapo juhudi za kuwajumuisha wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii hazitaleta tija-yaliyotokea Cologne ni ushahidi wa kutosha-kansela ndie atakaelazimika kuamua."

Poland yatishia mfumo wa dola linalofuata sheria

Na hatimae hatua za serikali ya kihafidhina ya Poland za kuifanyia marekebisho sera ya vyombo vya habari zinazusha mabishano ndani na nje ya nchi hiyo mwanachama wa Umoja wa ulaya. Gazeti la "Thüringer Allgemeine" linasema miongoni mwa nchi za nje, Ujerumani hasa ndiyo ambayo serikali ya Poland haitaki iikosoe. Kundi la Kaczynski linataraji kupata uungaji mkono wa mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya ambayo hayapendezewi kuiona Berlin ikiendelea kuwa na usemi mkubwa katika masuala yanayohusu Ulaya. Mbinu hizo lakini za mtengano hazina nafasi ya kufanikiwa. Na hata Ujerumani inabidi nayo ijizuwie. Kuhusu suala la kuporomoka mfumo wa taifa linaloheshimu sheria nchini Poland,wapoland wenyewe ndio wanaobidi walishughulikie.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef