Felix Tshisekedi aongoza kwenye matokeo ya awali Kongo
26 Desemba 2023Mwenye kiti wa Tume ya uchaguzi CENI, Denis Kadima amesema tume hiyo haitosita kufuta baadhi ya matokeo ya uchaguzi iwapo udanganyifu utathibitishwa. Kadima amesema vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi hazikupangwa na CENI na amewatupia lawama baadhi ya wanasiasa ambao walijaribu kuiba kura kwa kushirikana na baadhi ya mawakala wa tume ya uchaguzi.
Soma pia: Upinzani Kongo wapanga kufanya maandamano kulalamikia kasoro za uchaguzi
Hadi jana Jumatatu baadhi ya maeneo yaliendelea kupiga kura, ikiwa ni siku tano baada ya uchaguzi kufanyika. Tume ya uchaguzi imeelezea hatua hiyo inalenga kuwapa fursa wapiga kura wote ambao vifaa vya uchaguzi vilichelewa kufikishwa kwenye maeneo yao tarehe 20 Desemba.
Soma pia: Kwa nini uchaguzi ni muhimu DR Kongo?
Tume ya Uchaguzi kufikia sasa imetangaza matokeo ya kura milioni 1.9, kati ya jumla ya wapiga kura milioni 44 waliojiandikisha. Na rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili anaongoza kwenye matokeo hayo ya awali.