1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA inahitaji mageuzi haraka iwezekanavyo

28 Desemba 2015

Wagombea wa urais wa FIFA Mwanamfalme Ali Bin Hussein wa Jordan na Gianni Infantino wamesema mageuzi yanahitajika katika shirikisho hilo ili liibuke kutoka kwa mgogoro mbaya kabisa kuwahi kulikumba katika historia yake

https://p.dw.com/p/1HUfX
FIFA Ali Bin Hussein
Picha: picture-alliance/dpa/A. Rain

Viongozi hao wawili wamezungumza pamoja katika mdahalo wakati wa Kongamano la kumi la kila mwaka la Kimataifa la Michezo nchini Dubai hapo jana.

Mwanamfalme Ali wa Jordan aliyeshindwa katika uchaguzi wa rais wa FIFA mwezi Mei mwaka huu, alizungumzia hamu yake ya kutekeleza mabadiliko katika shirikisho hilo la kandanda la kimataifa ikiwa atachaguliwa. "Nimesafiri sana na kuyatembelea mashirikisho ya kitaifa kote ulimwenguni na yana wasiwasi kuhusu hadhi ya FIFA. Kwangu mimi ilidhihirisha azma yangu ya kuhakikisha kuwa tunaiweka FIFA katika mahali pazuri na kwamba turudi kwenye mchezo wenyewe wa kandanda, na hilo ndio lengo langu linaloimarika kila siku".

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kandanda Ulaya – UEFA Infantino alielezea imani yake kuwa ni uongozi thabiti tu unaoweza kuleta mageuzi yanayohitajika katika FIFA "Nadhani tunachohitaji sasa hakika ni uongozi imara, kutekeleza mageuzi maramoja na nadhani uwezo huu bila shaka upo na nnataka sana kuonyesha hayo katika miezi michache ijayo".

Mwanamfalme Ali na Infantino ni wawili kati ya wagombea watano wanaotaka kumrithi Rais wa FIFA Sepp Blatter katika uchaguzi maalum wa Februari mwakani, huku aliyekuwa afisa wa FIFA Jerome Champagne wa Ufaransa, mfanyabiashara wa Afrika Kusini Tokyo Sexwale na rais wa Shirikisho la Kandanda barani Asia Sheikh Salman Bin Ebrahim al Khalifa wa Bahrain wakikamilisha orodha hiyo ya wagombea.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Mohammed Khelef