FIFA yachapisha ripoti ya Garcia
28 Juni 2017Urusi na Qatar zinasema ripoti hiyo imethibitisha kuwa hakukuwa na makosa yoyote kwa upande wao. FIFA awali ilikuwa imekataa kuchapisha kikamilifu ripoti hiyo ya kurasa 430 kuhusiana na utoaji wa haki za kuandaa Kombe la Dunia nchini Urusi na Qatar iliyotayarishwa na mchunguzi huru Michael Garcia.
Lakini sasa shirikisho hilo la kandanda limelazimika kuitoa baada ya gazeti la Ujerumani Bild kusema kuwa limepata ripoti kamili na likachapisha kwa sehemu hapo jana, ikiwa ni pamoja na ufichuzi kuwa binti wa umri wa miaka 10 wa mmoja wa wanachama wa FIFA alipokea dola milioni mbili kwenye akaunti yake. FIFA inasema ilikuwa tayari inatafakari kuzindua ripoti hiyo kwa ukamilifu kabla ya uvujaji wa karibuni.
Katika ripoti hiyo ya mchunguzi mkuu wa FIFA Garcia kutoka mwaka wa 2014, kulikuwa na mtiririko wa fedha kutoka Qatar au mawakala hadi kwa wanachama wa kamati kuu ya FIFA, lakini haukuweza kuthibitishwa kuwahusisha waandaji wa Kombe la Dunia.
Garcia hakutaja ukiukaji wowote mkubwa uliofanywa na waandaji wa Urusi katika mchakato huo wenye utata. Hata hivyo mchunguzi huyo alisema maafisa wa FIFA na familia zao walipewa zawadi na vitu vingine vinono kama vile ziara za ikulu ya Urusi na kumbi za densi ya balle. Vitu hivyo havikuwa kinyume cha kanuni za maadili ya FIFA. Hata hivyo kompyuta za kamati ya Kombe la Dunia ya Urusi ziliharibiwa katika wakati wa uchunguzi. Wachunguzi hawangeweza kukusanya tena nyaraka zilizopotea.
Urusi na Qatar zimeikaribisha ripoti hiyo zikisema imethibitisha kuwa hazikufanya makosa yoyote kwa upande wao. Naibu waziri mkuu na Mkuu wa Urusi na mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Kombe la Dunia Vitaly Mutko amesema Urusi haikufanya chochote ambacho kinakiuka kanuni za maadili au utaratibu wa kawaida na misingi ya sheria za kutuma maombi.
Maafisa wa Qatar wamesema ripoti ya Garcia inathibitisha uadilifu wa zabuni yao. Ijapokuwa wamezusha maswali kuhusu muda ambao uvujaji wa ripoti hiyo umefanywa.
Uamuzi wa kuchapisha ripoti hiyo ulitolewa na kamati ya maadili chini ya uongozi mpya wa Maria Claudia Rojas wa idara ya uchunguzi na Vassilios Skouris wa idara ya kutoa maamuzi.
FIFA imesema kwenye tovuti yake kuwa inakaribisha habari za kuchapishwa kikamilifu ripoti hiyo. imesema hatua hiyo ilikuwa imeitishwa mara kadhaa na rais wake Gianni Infantino. Imeongeza kuwa wakuu wa zamani wa kamati ya maadili, Cornel Borbely na Hans-Joachim Eckert mara zote walikataa kuichapisha.
Hata hivyo Borbely na Eckert walisema katika taarifa kuwa uamuzi wa kutochapicha ripoti hiyo uliheshimu sheria za FIFA kwa sababu baadhi ya kesi zilizotajwa kuhusiana na ripoti hiyo zilikuwa bado zinaendelea.
Garcia alijiuzulu Desemba 2014 katika hatua ya kulalamikia uamuzi wa FIFA kutochapisha ripoti hiyo na pia kwa kutokubaliana na muhtasari wa ripoti iliyochapishwa na Eckert, ambayo iliiondolea makosa Qatar.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi ssessanga