1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA yaidhinisha timu 48 kwenye Kombe la Dunia

10 Januari 2017

Shirikisho la Soka la Kimataifa, FIFA limekubaliana kuongeza idadi ya timu zitakazoshiriki michuano ya Kombe la Dunia hadi 48, kutoka idadi ya sasa ya 32

https://p.dw.com/p/2VaFB
Schweiz Zürich FIFA Logo am Hauptquartier
Picha: picture-alliance/dpa/S. Schmidt

Shirikisho hilo la soka duniani, limeandika kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba baraza lake ambalo ndilo chombo cha  maamuzi limekubaliana kwa kauli moja kuufadhili mpango huo wa mabadiliko yatakayoanza katika mashindano yajayo ya Kombe la Dunia mwaka 2026.

FIFA imesema muundo huo mpya utahusisha raundi ya kwanza ya makundi 16 yakiwa na timu tatu, na timu mbili za juu zitaendelea hatua ya 32.  

Rais wa FIFA, Gianni Infantino aliyechukua nafasi hiyo kutoka kwa Sepp Blatter mwezi Februari mwaka jana ametimiza ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni za kugombea nafasi hiyo, ya kulipanua Kombe la Dunia. Awali Infantino alipendekeza kuwepo timu 40, na baadae aliongeza timu 8.

Mchezaji nguli wa zamani wa timu ya taifa ya Argentina, ambayo imekuwa ikishiriki michuano hiyo Diego Maradona amesema ni hatua muhimu hasa kwa mataifa ambayo hayajawahi kushiriki michuano hiyo.

Kuongezeka kwa timu hizo 16 kuna maanisha kwamba kutakuwa na mechi 80, badala ya 64. FIFA inatabiri kwamba watahitaji angalau mapato ya Dola bilioni 1 zaidi kupitia matangazo kwenye vyombo vya habari, mikataba na wafadhili, pamoja na mauzo ya tiketi, ikilinganishwa na makadirio ya mapato ya Dola bilioni 5.5 kwa ajili ya mashindano hayo mwaka 2018 nchini Urusi. 

Schweiz FIFA Gianni Infantino
Rais wa Shirikisho la soka la kimataifa, FIFA Gianni InfantinoPicha: Getty Images/M. Hangst

FIFA inataraji kuongeza kiwango cha faida cha Dola milioni 640, pamoja na gharama za ziada ya uendeshaji na fedha za zawadi kwa timu shiriki.

Afrika na Asia zataraji kunufaika zaidi.

Afrika Mashariki na Kati hazijawahi kutoa timu kushiriki michuano hiyo mikubwa duniani. Mdau wa soka nchini Tanzania Mtemi Ramadhan anasema ni jambo jema sana kwa kuwa ni wazi kwamba washiriki kutoka afrika sasa wataongezeka na kuongeza ushindani kwenye michuano hiyo.

Shirikisho la soka Barani Ulaya UEFA linataka timu 16 kushiriki michuano hiyo, inayotarajiwa kuchezwa Marekani ya Kaskazini. Shirikisho la Soka la Marekani Kaskazini, Kati na Carribean, CONCACAF halijawa kuandaa michuano hiyo tangu mwaka 1994, ilipofanyika nchini Marekani. Viongozi wa soka wa Marekani, Canada na Mexico wamekuwa na mazungumzo yasiyo rasmi ya kuandaa michuano hiyo kwa pamoja.

Afrika na Asia wanaweza kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kupata hadi nafasi tisa kwa kila moja. Walikuwa na timu tano tu ama nne mwaka 2014 nchini Brazil.

Pamoja na kuongezeka michezo 16, FIFA inaamini idadi ya viwanja itasalia kuwa ile ile, yaani viwanja 12 vilivyotumiwa na Urusi na Brazil. Lakini kuongezeka kwa mahitaji ya vituo vya mafunzo na hoteli kuna maanisha kwamba nchi zinazoendelea zina nafasi finyu ya kuwa wenyeji wa michuano hiyo kwa siku zijazo.  

Mwandishi: Lilian Mtono./AFPE/RTRE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo