1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA yaipiga marufuku Kenya katika soka ya kimataifa

Shisia Wasilwa
25 Februari 2022

Shirikisho la Kandanda Ulimwenguni, FIFA,limeipiga marufuku Kenya kutokujihusisha na masuala yoyote ya mpira wa miguu ya shirika hilo,kutokana na uingiliaji kati wa serikali.

https://p.dw.com/p/47a4i
Kenia Nairobi | Spieler Mali | Qualifikation FIFA World Cup 2022
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Akitoa tangazo hilo, Infantino ametoa shuruti kwa taifa la Kenya kuondolewa marufuku hiyo ni kwanza serikali irejeshe uongozi wa Shirikisho la Kandanda lililovunjwa na kamati ya muda iliyoteuliwa ivunjwe mara moja.

"Imetulazima kupiga marufuku wanachama wetu wawili: Kenya and Zimbabwe, kwa sababu ya serikali kuingilia katika masuala yao ya kandanda. Mashirikisho ya mataifa hayo yamepigwa marufuku katika masuala yoyote ya kandanda. Utekelezaji wake unaanza mara moja na mataifa hayo yanafahamu kinachostahili kufanywa ili yarejeshwe ama marufuku kuondolewa.”,alisema Infantino.

Marufuku hii inamaanisha kuwa Kenya haiwezi kucheza katika mashindano yoyote ya kimataifa ama hata marefa wake kusimamia mechi zozote za kimataifa. Kwa upande wake, Zimbabwe ilipigiwa marufuku baada ya Tume yake ya Michezo kukataa kuachia uongozi Shirikisho la Kandanda la taifa hilo - ZIFA. Maafisa wa ZIFA walitimuliwa afisini mwezi Novemba kwa tuhuma za ufisadi. 

Soma pia→Kenya imeivunja bodi ya soka kwa tuhuma za rushwa

Uingiliaji wa serikali

Infantino amesema hatua hiyo imetokana na Kenya kuingilia kati masuala ya kandanda nchini humo
Infantino amesema hatua hiyo imetokana na Kenya kuingilia kati masuala ya kandanda nchini humoPicha: picture-alliance/dpa

Tangazo hilo linajiri juma moja tu baada ya timu ya taifa ya wanawake, Harambee Starlets, kuondolewa kwenye mashindano ya kuwania Kombe la Afrika la Wanawake ilipokuwa icheze dhidi ya Uganda. Mechi hiyo ilikuwa imeratibiwa kuchezwa tarehe 17 mwezi huu.

Barry Otieno aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Kandanda lililovunjwa aliandika barua kwa Shirikisho la Kandanda barani Afrika, CAF akitaka hatua hiyo kuchukuliwa.

Meli ya kandanda nchini Kenya ilianza kuvuja tarehe 11 mwezi Novemba mwaka uliopita baada ya waziri wa Michezo, Amina Mohamed, kulivunja Shirikisho la Kandanda la Kenya na badala yake kuteua kamati ya kusimamia kandanda kwa kipindi kifupi.

Soma pia→Kenya kuadhibiwa na FIFA?

Tuhuma za FIFA

Rais wa Shirikisho la Kandanda nchini, Nick Mwendwa, akituhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha na ofisi, alitiwa nguvuni mara mbili na kushtakiwa kwa makosa manne ya kupata mali kwa njia ya udangayifu na nyingine ya ufisadi.

Hata hivyo FIFA ilisema kuwa haingeingilia uchunguzi huo na kuelezea kuwa haiungi mkono ufisadi. Kwa sasa mataifa ya Kenya na Zimbabwe hayatapata ufadhili wowote kutoka kwa FIFA hadi yatatue migororo katika mchezo wao wa kandanda.