1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Frankfurt yajiimarisha katika nafasi ya tat

6 Februari 2017

Kinyang'anyiro cha kutafuta nafasi ya kucheza kandanda la Ulaya msimu ujao kinaendelea kupamba moto katika ligi ya Ujerumani - Bundesliga

https://p.dw.com/p/2X3Tq
Deutschland Eintracht Frankfurt - Darmstadt 98  | Makoto Hasebe
Picha: picture alliance/dpa/F. Rumpenhorst

Eintracht Frankfurt waliwafunga washika mkia Darmstadt 2-0 na kupanda hadi nafasi ya tatu juu ya Borussia Dortmund. Frankfurt ambao walicheza fainali ya Kombe la Ulaya mwaka wa 1960, wako katika harakati za kucheza kandanda la Champions League kwa mara yao ya kwanza msimu ujao baada ya ushindi wao wa jana kuwaondoa katika nafasi ya saba.

Katika mchuano wa mapema jana, Augsburg iliifunga Werder Bremen 3-2. Ushindi huo uliwaweka Augsburg katika nafasi ya kumi kutoka ya 15 wakati Bremen wakibakia katika vita vya kushuka daraja.

Vijana wa Carlo Ancelotti walilazimishwa kutoka sare ya 1-1 na Schalke na wana sababu ya kuwashukuru Dortmund ambao waliwashinda Leipzig bao moja kwa sifuri.

Kinyang'anyiro cha kutafuta nafasi ya kandanda la Ulaya kinapamba moto, maana Frankfurt wana pointi 35, wakati Borussia Dortmund, Hoffenheim zikiwa na pointi 24 kila mmoja, Hertha Berlin ina 33 na Colgone 32. Bayern Munich wanaongoza kileleni na pointi 46 wakifwatwa na RB Leipzig na 42.

Premier league

Kule England, Kama tu ilivyo hapa Ujerumani, kinyang'anyiro cha kutafuta nafasi za Champions League msimu ujao kinashika kasi. Manchester City walipata ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Swansea wakati Manchester United wakiwaadhibu Leicester 3-0.

Ni pointi tano zinazotenganisha timu nambari mbili Tottenham Hotspur na nambari sita Manchester United. City ilisonga hadi nafasi ya tatu juu ya Arsenal na Liverpol. Wakati kama huu msimu uliopita, Leicester ilikuwa inaongoza ligi kuelekea katika ubingwa wao wa kwanza kabisa katika historia.

Lakini mambo yamebadilika kabisa msimu huu maana baada ya kupoteza mechi 13 kati ya 24, vijana hao wa kocha Claudio Ranieri wako pointi moja juu ya eneo la kushushwa ngazi, na wanakabiliwa na kitisho cha kuwa bingwa mtetezi wa kwanza kushushwa daraja tangu Manchester City katika msimu wa 1937-38.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP
Mhariri: Gakuba Daniel