1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G-20 haitarudisha nyuma nyuma makubaliano ya Paris

29 Juni 2017

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema ulimwengu hauwezi kurudi nyuma wala kuyajadili kwa mara ya pili Makubaliano ya Paris kuhusiana na tabia nchi.

https://p.dw.com/p/2fcgs
Deutschland Bundestag Angela Merkel
Kansela Angela Merkel akiwa katika bunge la Ujerumani AlhamisPicha: Reuters/F. Bensch

Akizungumza katika bunge la Ujerumani, Bundestag, Alhamis, wiki moja kabla ya mkutano mkuu wa mataifa 20 yaliyostawi kiviwanda duniani G20 utakaoandaliwa mjini Hamburg, Merkel alisema wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya waliosalia wameonesha kuunga mkono mpango huo wa kusitisha mabadiliko ya tabia nchi, licha ya Marekani kuamua kujiondoa katika makubaliano hayo.

Katika kauli aliyoonekana kuielekeza kwa Rais Donald Trump wa Marekani, Kansela huyo wa Ujerumani amesema wale wanaoamini kwamba matatizo ya dunia yanaweza kusuluhishwa kupitia mtindo wa kutenga na kujilinda, wamekosea pakubwa kwani changamoto kuu zitasuluhishwa tu kupitia umoja.

Hatua ya uongozi wa rais Trump ya "Marekani kwanza" au kuipa Marekani kipau mbele kuliko mataifa mengine katika biashara na hata masuala mengine, ni jambo lililozua wasiwasi mkubwa pamoja na uamuzi wake wa kujiondoa katika yale makubaliano ya tabia nchi ya Paris.

Merkel atakutana na viongozi wengine wa G-20

"Umoja wa Ulaya hautayumba kamwe katika yale makubaliano ya Paris na kwa haraka, Umoja huu utayatekeleza kwa pamoja yaliyomo," alisema Merkel. "Fauka ya hayo, tangua Marekani itangaze uamuzi wa kujiondoa katika makubaliano hayo, tumepata nguvu zaidi ya kuhakikisha kwamba tunafanikiwa katika utekelezaji wa makubaliano hayo."

Deutschland G-20 Hamburg Gefangenensammelstelle
Kunatarajiwa maandamano mkutano huo wa G20 utakapoanza Picha: picture-alliance/M. Scholz

Baadae Alhamis, Merkel atakuwa anakutana na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May kisha baada ya hapo akutane na viongozi wa G20 kwa matayarisho ya huo mkutano mkuu wa wiki ijayo.

Kiongozi huyo wa Ujerumani atakuwa mwandalizi wa mkutano huo tarehe 7 na 8 mwezi Julai, mkutano utakaowaleta pamoja viongozi kama Trump, rais wa Urusi Vladimir Putin na rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan.

Merkel anasema G20, muungano uliopata umaarufu baada ya ule mfumuko wa bei ulioikumba dunia, una umuhimu mkubwa mno sasa, kwasababu nchi zinazofanya kazi pamoja zinaweza kubadilisha mambo kwa njia bora kuliko sera za kitaifa ambazo hazina ushirikiano wa aina yoyote.

Merkel pia anataka kuungwa mkono katika suala la masoko huru

"Shabaha niliyojiwekea katika mkutano mkuu wa G20," alisema Merkel, "ni ishara ya umoja ambayo viongozi wa G20 wataonesha kuelewa jukumu lao kubwa kwa dunia na walifanyie kazi jukumu hilo."

Türkei Putin und König Salman bin Abdulaziz Al Saud
Rais wa Urusi Vladimir Putin pamoja na Mfalme Salman wa Saudi Arabia watahudhuria mkutano wa G20 Hamburg Picha: picture alliance/dpa/M. Klimentyev

Merkel pia amesema anatarajia uungwaji mkono katika suala la masoko huru na ufanyaji biashara ya mataifa mbali mbali duniani katika mkutano huo wa Hamburg wiki ijayo.

"Naamini kwamba suala la kujilinda haliwezi kuwa suluhu. linamdhuru kila mmoja na ndiyo sababu tunahitaji masoko huru," alisema Merkel. "Lengo langu kwa hiyo ni mkutano huu utoe ishara ya wazi kwa masoko huru na vigingi vilivyoko pamoja na kujitolea kwao kwa mfumo wa biashara wa mataifa mengi."

G20 ni muungano unaojumuisha mataifa ya Argentina, Brazil, China, Ujerumani, Ufaransa, Urusi, Saudi Arabia, Afrika Kusini na Marekani miongoni mwa mataifa mengine pamoja na yale yaliyoko katika Umoja wa Ulaya. Nchi nyengine zitakazohudhuria mkutano wa mwaka huu ni Norway, Uhispania, Guinea, Senegal, Singapore na Vietnam.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFPE/DPAE

Mhariri: Mohammed Khelef